BAADA ya kuwa na matokeo mazuri msimu huu ukilinganisha na miaka ya nyuma, Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda, amesema malengo yake ni kumaliza Ligi Kuu Bara wakiwa ndani ya nafasi tano za juu.
Coastal Union ambayo imecheza mechi 28, ina pointi 46 na katika msimamo wa ligi iko kwenye nafasi ya nne nyuma ya vinara Simba wenye 71, Azam FC ( pointi 54), Yanga (pointi 51) na Namungo FC yenye pointi 50.
Mgunda alisema kikosi chake kimeshaanza mazoezi ya pamoja na amefurahishwa na kasi ambayo amewakuta nayo wachezaji wake.
Kocha huyo alisema mechi zilizobakia katika Ligi Kuu Bara ni chache lakini lolote linaweza kutokea kwa watakaofanya vizuri na watakaoharibu.
"Tumejipanga, lengo ni kumaliza msimu tukiwa katika nafasi tano za juu, tunaamini hili linawezekana kama hatutabweteka, ligi ni ngumu na huku tunakoelekea ndio pagumu zaidi," Mgunda alisema.
Aliwataka wachezaji wake kuendeleza 'moto' waliouwasha katika mzunguko wa kwanza ili kujiweka kwenye nafasi salama.