Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Coastal Union yaifundisha Biashara Ligi Kuu ilivyo

13964 Costal+pic TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Mshambuliaji Haji Ugando ameiwezesha Coastal Union ya Tanga kuondoka na pointi tatu katika mchezo wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Ushindi wa Coastal Union dhidi ya Biashara umeifanya timu hiyo ya Tanga kukaa kileleni mwa msimamo ikifikisha pointi nne na kuishusha Azam iliyokuwa ikiongoza.

Ugando alilifunga katika dakika ya 20 baada ya kuwaahada mabeki wa timu pinzani na kupiga shuti kwa mguu wa kushoto lililotinga wavuni.

Kabla ya bao hilo katika dakika ya 12 mwamuzi aliizawadia penalti Coastal Union ambayo ililalamikiwa na wachezaji wa Biashara kwa kuwa mchezaji wa Coastal alianguka peke yake lakini mwamuzi akasisitiza kuwa aliguswa. Hata hivyo kipa aliipangua na mpira kuokolewa.

Katika dakika ya 45 vijana wa Biashara walipata faulo iliyopigwa moja kwa moja lakini baada ya kujaa wavuni mwamuzi akalikataa bao hilo akisema kuwa kuna mchezaji wa Biashara aliotea kabla ya mpira huo kupigwa jambo lililolalamikiwa na wachezaji hao ambao ilibidi benchi la ufundi liwatulize.

Hata baada ya kipenga cha kuashiria mapumziko wachezaji wa Biashara bado walimzonga mwamuzi na mshika kibendera kwa kulikataa bao lao.

Katika kipindi cha pili timu zote zilishambuliana kwa zamu lakini kwa kiasi kikubwa ubabe ulitawala na kutibua burudani hiyo.

Hadi dakika 90 zinakamilika ushindi ulikuwa ni wa Coastal Union ambayo imeongoza Ligi kwa muda kuzisubiri mechi za leo, timu hiyo imefikisha pointi nne kwa michezo miwili yote ikicheza katika uwanja wake wa nyumbani, mechi ya kwanza ilitoka 1-1 na Lipuli FC ya Iringa.

Nayo Biashara licha ya ugeni wake katika Ligi hiyo ilivuna pointi tatu kutokana na kushinda mechi ya kwanza iliyocheza ugenini dhidi ya Singida United kwenye uwanja wa Namfua, mjini Singida.

Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa jana, wenyeji Singida United, walizinduka na kujipatia pointi tatu baada ya kuwalaza Mwadui FC ya Shinyanga kwa bao 1-0.

Bao pekee katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida lilifungwa na mlinzi Rajab Zahir.

Chanzo: mwananchi.co.tz