Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chondechonde Taifa Stars isigeuzwe mtaji wa kisiasa

49515 Pic+stars

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hoja kwamba siasa na soka ni mapacha hutafsiriwa kwa mifano rahisi; kwamba mchezaji wa zamani wa Algeria, Ahmed Ben Bella aligeuka mwanasiasa na kuwa Rais wa nchi hiyo.

Au nyota wa zamani ya timu ya Taifa ya Visiwa vya Faroe, Kaj Leo Johannesen alichaguliwa kuwa waziri mkuu kabla ya kung’olewa mwaka 2015.

Mfano maarufu zaidi duniani ni mchezaji bora wa zamani wa dunia wa Fifa na mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or, George Weah aliyechaguliwa kuwa Rais wa Liberia mwaka 2017. Weah pia alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ulaya na Afrika katikati ya miaka ya tisini.

Hata hivyo, upacha wa soka na siasa hupigwa marufuku kwa sababu ya hulka za wanasiasa kutumia majukwaa ya kijamii kujipatia mtaji wa kisiasa. Fainali za Kombe la Dunia mwaka 1978, aliyekuwa dikteta wa Argentina, Jorge Videla, aliitumia michuano hiyo kuuonyesha ulimwengu kuwa nchi hiyo ni tulivu na wananchi ni wamoja. Fainali hizo zilifanyika Argentina.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa kutambua hilo la siasa kupenyezwa kwenye soka ndiyo maana katika orodha ya sheria za mchezo, sheria namba 4 imepiga marufuku alama na ujumbe wa siasa kwenye vifaa vya lazima kwa wachezaji ndani ya uwanja. Sheria hiyo inakataza pia udini na ujumbe au alama binafsi.

Fifa hawaishii tu ndani ya uwanja, bali wanakataza shughuli za uendeshaji wa soka kuingiliwa na siasa wala Serikali. Mantiki ni kwamba soka ni mchezo, vilevile ni burudani hivyo inatakiwa kuunganisha watu kuliko kuwagawa wakati siasa ni itikadi. Popote palipo na itikadi lazima mgawanyiko utokee.

Mathalani, chama fulani kinapokuwa kinaendesha timu ya soka, kuna watu wataipenda kwa sababu tu ni ya chama chao lakini wapo watakaoichukia kwa kigezo tu ni timu ya chama wasichokubaliana nacho kiitikadi. Huo ndiyo mgawanyiko ambao hautakiwi.

Kutumia soka kujinufaisha kisiasa ni dhambi kwa nchi, zaidi ni kuukosea mchezo wenyewe. Mchezo unapokutanisha timu zenye uhasama wa kisiasa huondoa tafsiri ya mchezo na kusababisha chuki ziingie katikati. Soka lina lugha zake. Wapinzani katika soka huzungumza kwa namna yao.

Taifa Stars inavamiwa

Kila Mtanzania anapaswa kufurahi baada ya Taifa Stars kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Ushindi wa mabao 3-0 ambao Taifa Stars iliupata dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, kisha Cape Verde kutoka suluhu na Lesotho, ni matokeo yaliyoifanya Stars kumaliza nafasi ya pili katika kundi L, nyuma ya Uganda. Stars inakwenda Afcon kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 1980. Mashindano hayo yalifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1957.

Lugha za kabla na baada ya mchezo ndizo zinasababisha kuonekana siasa zinaivamia Taifa Stars. Katika posti niliyoweka Facebook kuhamasisha watu kwenda uwanjani kuishangilia Stars dhidi ya Uganda mmoja wa waliochangia alisema: “Sasa hivi tunaambiwa ni timu yetu, Taifa Stars ikifuzu tutaambiwa ni utekelezaji wa ilani ya chama chao.”

Baada ya mechi, katibu wa uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, aliandika kwenye akaunti yake ya Twitter kuwa mabao matatu ambayo Stars walipata dhidi ya Uganda, yanagawanyika katika miradi mikubwa mitatu; mosi, ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), pili, ni mradi mkubwa wa umeme wa Stiegler’s Gorge na tatu ni ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Mwisho wa ujumbe wake, Polepole alisema ushindi wa Stars unaendana na utekelezaji wa ilani ya CCM. Kumbuka kuwa kuna mtu alitanguliza hofu yake mapema kuwa Taifa Stars ikifuzu kuna chama kitajisifu kwamba kinatekeleza ilani, halafu Polepole ametamka yaleyale.

Meya wa Ubungo (Chadema), Boniface Jacob baada ya mechi ya Stars na Uganda, aliipongeza Taifa Stars kwa ushindi, kisha akasema kuwa kuna chama kilifanya tambo makusudi ili kuwakasirisha (wapinzani) wasuse na wasiiunge mkono Taifa Stars, lakini waliukwepa huo mtego na kushiriki kuiombea na kwenda uwanjani kuishangilia.

Haya ndiyo mambo ambayo yanapaswa kukemewa. Taifa Stars haipaswi kuonekana wakati wowote inafungamana na chama chochote cha siasa.

Na vyama vya siasa kwa ajili ya kutenda haki visijionyeshe kimbelembele kwenye timu kwa namna yoyote ile. Taifa Stars ni ya Watanzania wote.

Timu inakwenda Misri, siasa ziwekwe kando. Watanzania wawe wamoja katika kuiunga mkono timu yao.

Watu na vyama vyao wakiwa kwenye majukwaa na ofisi zao, wanapoielekea Taifa Stars itamkwe tu ni Watanzania na siyo chama fulani.

Hilo halikubaliki katika soka kwa sababu haina afya kwa mustakabari wa Tiafa letu.

Chanzo: mwananchi.co.tz