WAKATI Kocha Mwinyi Zahera akiipa Yanga ramani ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara, aliyekuwa straika wa timu hiyo, Obrey Chirwa amewatumia ujumbe mabosi wake wa zamani kuwa anataka kuvunja mkataba wake kule Misri ili tu arudi Jangwani.
Mzambia huyo amefichua kuwa anataka arejee Jangwani na kukipiga japo kwa mwaka mmoja, kwani muda mfupi tu aliotimka Yanga amejikuta akiwamisi kinoma, hivyo kuomba wamfungulie mlango mapema kipindi hiki.
Chirwa amewasilisha maombi hayo kwa njia ya sauti kwa mtandao akiwaambia Yanga wazungumze na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika ili kumpa nafasi tena na kuja kukipiga Jangwani.
Katika ujumbe huo ambao Mwanaspoti limeunasa, Chirwa amewaambia Yanga kuwa klabu yake ya sasa haijamlipa fedha za usajili na anafikiria kuvunja mkataba nao kabla mambo hayajaharibika huko Misri.
Straika huyo aliongeza, makubaliano na mabosi wa klabu hiyo juu ya malipo hayo muda umepitiliza na anaona ni bora arudi Tanzania ambako alishaizoea, pia ni jirani na kwao Zambia tofauti na Misri iliyopo Kaskazini mwa Afrika.
Aliongeza kuwa iwapo Nyika na kamati yake itakubali yuko tayari kurudi na kusaini mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Kutokana na hilo, Mwanaspoti lilimtafuta Nyika ambaye alikiri kupata ujumbe huo lakini akasema kwa sasa hawawezi kulizungumzia kwani usajili wao kwa sasa unaanzia kwa mapendekezo ya benchi la ufundi.
“Nimetumiwa hiyo sauti nimeisikia, tunashukuru kusikia wachezaji wengi waliondoka Yanga wanatamani kurudi hapa, ila kwa sasa hilo la Chirwa kutaka kurudi halina nafasi kwetu kwa kuwa usajili wetu siku zote umekuwa unaanzia kwa makocha na sio sisi kama viongozi,” alisema Nyika.
Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Yanga, ambaye kwa sasa yupo DR Congo na kesho Jumatatu anaianza safari ya kwenda Liberia kwa ajili ya mchezo wao wa kuwania fainali za Afcon 2019, amekiangalia kikosi chake na kuwapa mabosi wa Jangwani mchongo ambao wakiufanyia kazi, lazima taji la Ligi Kuu Bara lilirudi Jangwani.
Zahera aliliambia Mwanaspoti ameiona Simba na anaamini kama mabosi wake watatuliza akili na mipango yao na kuyafanyia kazi mambo mawili basi anaweza kurudisha mataji yote yaliyopotea.
Zahera alisema mara atakaporudi na uongozi utahakikisha anawapata wachezaji wake na kukaa nao pamoja kazi ya kutafuta ubingwa itakuwa rahisi na liko ndani ya uwezo wake.
Mkongomani huyo alisema kama Yanga itaendelea kuwakosa wachezaji wake kwa nyakati tofauti kutokana na sababu za kiutendaji linaweza kuwapunguzia ubora ambao wameanza nao.
“Tuna timu nzuri, kwa sasa akili yetu itakuwa ni ligi hii ni nafasi nzuri kwetu tutapata muda mzuri wa kujiandaa mechi moja kwenda nyingine,” alisema.
“Kama uongozi utaweza kuhakikisha akili ya wachezaji inabaki katika timu na sio leo hawa hawapo wale wapo, basi kupata mafanikio hilo litakuwa ndani ya uwezo wetu,”