Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chilunda ndani ya CD Tenerife

11648 Pic+chilunda TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mshambuliaji wa Tanzania, Shaaban Idd Chilunda ameanza maisha yake mapya nchini Hispania kwenye klabu yake ya CD Tenerife itakayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini humo ambayo ni maarufu kama Segunda.

Chilunda ambaye aliibuka kuwa mfungaji bora wa michuano ya Kagame mara baada ya kutua Hispania alifanyiwa utambulisho mbele ya vyombo vya habari nchini humo.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Azam, Shabaan alitambulishwa Agosti 10 katika hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi Hatusa (Red Volkswagen Canarias).

Chilunda amesaini mkataba wa mkopo wa miaka miwili CD Tenerife na mchana wa Agosti 11 alifanya mazoezi yake ya kwanza kwenye kituo cha Ciudad Deportiva Javier Perez.

Akizungumza mbele ya wanahabari, Chilunda katika utambulisho wake amesema ni faraja kwake kujiunga na klabu hiyo.

“Nilikuwa mwenye furaha kubwa tangu niliposikia CD Tenerife wananitaka nijiunge nao.

“Nipo katika kiwango kizuri na natambua kuwa mazoezi yatakuwa tofauti na yale niliyokuwa nafanya nyumbani Tanzania, lakini haitokuwa vigumu kwangu kuzoea kwa sababu nipo tayari kwa maisha mapya.

“Mimi ni mshambuliaji sipo hapa kwa ajili ya kufunga tu, nipo hapa kwa ajili ya kushirikiana na wenzangu, nitasaidia kutengeneza nafasi za kufunga na kila kitu kinatakachokuwa ninaelekezwa kufanya,” anasema Chilunda.

Anaendelea kwa kusema; “Nitajitoa kwa ajili ya wenzangu ninaamini haitachukua muda kuzoea hapa na kufanya kile ninachoelekezwa na kocha wangu.”

“Nitacheza kwa nguvu na kwa kiwango kizuri, hilo siyo tatizo kwangu, japokuwa najua Hispania itakuwa tofauti, ila nitazoea kwa haraka.”

“Faridi (Mussa) ni mfano mzuri kwangu, ninavyomuana nacheza sasa ni tofauti ilivyokuwa kabla,” anasema Chilunda katika mkutano huo mbele ya wanahabari.

Mkurungezi wa ufundi wa CD Tenerife, Alfonso Serrano naye ametia neno kwa kusema Chilunda yupo hapo kwa mkopo wa miaka miwili akionyesha kiwango cha juu basi watamnunua moja kwa moja.

“Tuna imani na kiwango chake na rekodi yake ataanza kucheza katika mechi ya Agosti 17 na tutamuangalia jinsi anavyozoea hapa hadi Desemba.

“Chilunda hakuja hapa kufanya majaribio, tutachukua uamuzi juu yake kadri muda unavyokwenda, wawakilishi wake wametupa muda mrefu wa kukaa naye, alitakiwa kuwa hapa mapema ila urasimu umemchelewesha” alisema Serrano.

“Tuna imani naye, lakini hatutompa presha ya kuzoea hapa haraka tunaamini baada ya muda atakuwa sawa. Ni mwepesi ana uwezo mkubwa wa kufunga mabao,” anasema Serrano.

Baada ya mazungumzo hayo, Spoti Mikiki na yenyewe imefanya juhudi za kuwasiliana na Chilunda ambaye anaoneka kuwa mwenye furaha huku akisema hawezi kuichezea nafasi ambayo ameipata ndani ya klabu hiyo.

“Ndoto yangu ilikuwa ni kucheza Ulaya, nilijipa muda kwa kujifunza mengi kutoka kwa kaka zangu, Mbwana Samatta na Saimon Msuva lakini pia Farid naye hakusita kunipa moyo.

“Nimekuwa na mawasiliano na Farid kwa kipindi kirefu kwa hiyo baada ya kupata hiyo nafasi amekuwa msaada kwa kuniambia nini cha kufanya ili kuendana na mpira wao,” anasema Chilunda.

Hata hivyo, Chilunda anasema kuwa Farid alimpa moyo kwa kumweleza ataweza kuendana na mpira wa Hispania kwa kipindi kifupi na kwa kuwa yeye ni mshambuliaji wa mwisho hatokuwa na mambo mengi.

Zaidi ya kufunga na kukaa kwenye nafasi, anasema kuwa ameelezwa beki wa kwanza kukaba ni mshambuliaji pindi na mpira wanapokuwa nao wapinzani.

Chilunda anadai kulitambua hilo tangu akiwa Azam na amekuwa akibadilika na kuwa beki wa kwanza kukaba pindi ambapo wapinzani wanapouanza mpira.

Kuhusu lugha, Chilunda anaamini taratibu atajifunza na mwishowe atakuwa kama Farid ambaye amekuwa na uwezo wa kukizungumza Kihispania japo sio cha ndani zaidi kama ilivyo kwa wazawa.

CD Tenerife ambayo itakuwa na Watanzania hao wawili kwenye msimu mpya wa Ligi Daraja la Kwanza unaotarajiwa kuanza Agosti 20, ilianzishwa mwaka 1912.

Timu hiyo inahistoria kubwa kwenye soka la Histania na Ulaya kwa ujumla, imewahi kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1996/97 kipindi hicho michuano hiyo ikiitwa kombe la UEFA.

Mafanikio mengine makubwa ambayo CD Tenerife imeyapata ni kutinga nusu fainali ya Copa del Rey mara moja ambapo ilikuwa msimu wa 1993/94 huku wakiishia katika hatua ya robo fainali mara nne.

Robo fainali hizo ilikuwa kwenye misimu ya 1960–61, 1961–62, 1975–76 na 1995–96.

Kama CD Tenerife itafanya vizuri msimu huu wa 2018/19 huenda washambuliaji wa Kitanzania, Farid Mussa na Shaaban Idd Chilunda wakacheza Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ msimu ujao.

Tenerife itaunza msimu wa daraja la kwanza Hispania kwa kucheza mchezo miwili ugenini wa kwanza utakuwa Agosti 20 dhidi ya Gimnàstic Tarragona na Agosti 26 dhidi ya Almería.

Chanzo: mwananchi.co.tz