Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chanzo cha waamuzi kufungiwa hiki hapa

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Wakati waamuzi wa soka wa Dar es salaam wakiendelea kung’ara kwenye mechi mbalimbali za kitaifa na kimataifa, mkosi wa kufungiwa umeendelea kuwatesa wenzao wa mikoani kabla hata Ligi Kuu Tanzania Bara haijafika raundi tano.

Rekodi zinaonyesha janga la kufungiwa limekuwa sugu kwa waamuzi kutoka nje ya Dar es Salaam huku likiwapitia mbali wenzao kutoka hapa jijini.

Uamuzi wa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwafungia waamuzi wanne kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kwenye baadhi ya mechi za raundi ya kwanza na pili msimu huu, umefanya idadi ya waamuzi waliofungiwa ndani ya mwaka huu kufikia wanane.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Chama, umebaini ukosefu wa mafunzo na mazoezi ya utimamu wa mwili ni chanzo cha waamuzi wa mikoani kushindwa kutafsiri vyema Sheria 17 za Mpira wa Miguu.

Katika orodha ya waamuzi wanane waliofungiwa tangu mwaka 2018 ulipoanza kwa kushindwa kutafsiri Sheria 17 za Mpira wa Miguu, hakuna mwamuzi wa Dar es Salaam aliyekumbana na kibano hicho.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema waamuzi wanne, Jimmy Fanuel, Nicholas Makaranga, Jamada Ahmada na Athuman Lazi kila mmoja amefungiwa kwa kipindi cha miezi mitatu kwa kuvunja kanuni ya 39(i) ya udhibiti wa waamuzi.

Wakati Fanuel akishindwa kutafsiri sheria kwenye mchezo wa Azam dhidi ya Mbeya City, Jamada alifanya hivyo kwenye mechi baina ya Singida United na Mwadui FC, Makaranga akichemsha katika mechi kati ya Ruvu Shooting na KMC sawa na mwenzake Athumani Lazi.

“Kamati ilikaa kikao cha kwanza Jumamosi kupitia taarifa za michezo ya raundi ya kwanza na pili, pia kutoa uamuzi juu ya masuala kadhaa ambayo yalionekana kwenda kinyume na kanuni na taratibu za ligi,” alisema Wambura.

Mbali na waamuzi hao, Wambura alisema waamuzi Nassor Mwinchui na Abdallah Rashid, shauri dhidi yao litachunguzwa zaidi kulingana na uzito wa malalamiko na ushahidi uliowasilishwa mbele ya kamati hiyo.

Kwa mujibu wa Wambura, kamati hiyo imewafungia miezi mitatu, makamishna Victor Mwandika na Juma Chaponda kwa kutoandika ripoti sahihi ingawa pia imewaonya mwamuzi Sylivester kutoka Kilimanjaro na makamishna Juma Msaka kwa kutotimiza majukumu yao.

Kufungiwa kwa waamuzi wanne ni muendelezo wa hadithi ya kufungiwa kwa wengine kutoka mikoani ndani ya mwaka huu ambapo hadi sasa jumla wamefikia tisa.

Januari 5, mwaka huu waamuzi wanne, Andrew Shamba, Abdallah Mkomwa na Athumani Athumani kutoka Pwani na Omari Juma (Dodoma) walifungiwa kwa kushindwa kutafsiri Sheria 17 za Mpira wa Miguu kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza baina ya Dodoma FC na Alliance.

Mwaka jana, waamuzi Ngole Mwangole kutoka Mbeya na Shakaile Ole Yangalai (Pwani) walikuwa miongoni mwa waamuzi waliokutana na adhabu ya kufungiwa kutokana na kushindwa kutimiza majukumu yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama aliliambia gazeti hili kuwa sababu inayochangia waamuzi wa mikoani kutofanya vizuri ni kutopata mafunzo ya mara kwa mara na mazoezi.

“Kutokana na kugundua tatizo sugu la waamuzi wa mikoani kushindwa kutafsiri sheria za mpira tumeandaa kozi kwa wakufunzi wa waamuzi,”alisema Chama.

Katika hatua nyingine, Prisons, Mbao FC na Coastal Union kila moja imetozwa faini ya Shilingi 500,000 kwa kosa la mashabiki wao kuvunja kanuni ya 43(i) inayotoa muongozo wa usimamizi na udhibiti wa klabu.

Pia Yanga, Mwadui na Singida zimepewa onyo kwa kuchelewesha kuwasilisha orodha ya wachezaji wao kwa ajili ya mechi tofauti na kanuni zinavyoelekeza.

Chanzo: mwananchi.co.tz