Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Chama, injini ya Simba iliyobadili gia angani

48540 CHAMA+PIC

Mon, 25 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Clatous Chama ndiye shujaa wa Simba. Ndio. Hakuna kama Chama katika kikosi hicho kinachoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dakika tatu za mwisho katika mchezo wa kuamua baina ya Simba na AS Vita ya DR Congo, zilimtambulisha kiungo huyo wa kimataifa wa Zambia ni mchezaji wa namna gani.

Bao la ushindi dakika ya 87, liliwaacha midomo wazi wachezaji wa AS Vita na mamia ya mashabiki wao waliokwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia mchezo huo.

Simba ilishinda mabao 2-1 na kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuvuna pointi tisa katika Kundi D ikiungana na vinara Al Ahly ya Misri.

Pamoja na bao hilo, kiungo huyo anatambulika kwa mambo makubwa manne anayofanya uwanjani.

Maarifa, uwezo binafsi, wepesi na nidhamu ya mchezo inamtambulisha Chama katika medani ya soka ingawa ni mchezaji anayecheza taratibu uwanjani.

Aina ya uchezaji wa Chama huwezi kuitofautisha sana na viungo nguli wa zamani Said Mwamba ‘Kizota’, Athumani China au Hamisi Gaga ‘Gagarino’.

Simba haikukosea kumsajili akitokea Dynamos ya Zambia. Pia amewahi kuzitumikia kwa nyakati tofauti Ittihad ya Misri na Zesco United ya Zambia.

Pamoja na umahiri wake wa kutawala eneo la katikati, kiwango cha Chama kimekuwa cha kupanda na kushuka katika Ligi Kuu Tanzania Bara na hata Ligi ya Mabingwa Afrika.

Haikushangaza baadhi ya mashabiki kumuhoji kupitia mtandao kuhusu uwezo wake usiotabirika uwanjani licha ya kuonekana ni mchezaji mwenye kipaji.

“Mchezaji hawezi kuwa katika kiwango kilekile siku zote, lakini nafanyia kazi maoni yenu kuhakikisha narejesha kiwango changu mlichozoea,” aliandika Chama akiwajibu mashabiki.

Bila shaka wadau wengi hawajui umuhimu wa Chama, lakini Kocha wa Simba Patrick Aussems humwambii kitu kuhusu Chama.

Kwa kutambua umuhimu wake, Aussems ameweka pamba masikioni na kuamua kujilipua kwasababu anajua ubora wake.

Nahodha huyo wa zamani wa Dynamos alianza kuibeba Simba Desemba 23 katika mchezo wa mwisho wa kutafuta nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia. Katika mchezo wa kwanza Simba ilikubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Nkana, ugenini mjini Kitwe na ilikuwa ikihitaji ushindi wa mabao zaidi ya mawili katika mchezo wa marudiano ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya makundi.

Timu hizo zikakutana Dar es Salaam na Simba ilishinda mabao 3-1 huku bao la tatu na lililioipeleka timu hiyo hatua ya makundi likifungwa kwa kisigino na Chama.

Achana na bao hilo alilofunga lakini pia alihusika katika mabao mengine mawili yaliyofungwa na Jonas Mkude na Meddie Kagere.

Pia Chama aliibeba tena Simba Machi 16 alipoiongoza kutinga robo fainali ya mashindano hayo kwa kuichapa AS Vita mabao 2-1.

Timu zote mbili zilikuwa na nafasi endapo zingeshinda mchezo huo na ilikuwa bahati kwa Simba kupata bao la jioni dakika ya 87 lililofungwa na Chama na kuipeleka robo fainali.

AS Vita ndio ilikuwa ya kwanza kufunga bao katika mchezo huo kabla ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuisawazishia Simba na wakati watu wakiamini mchezo huo ungemalizika kwa sare, Chama alifanya vitu vyake.

Mchambuzi Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’ anasema Chama anastahili kuwa mchezaji wa kulipwa. “Amekuwa msaada mkubwa kwa Simba mashambulizi yake yanaonekana kama sio ya hatari lakini ni hatari kwa sababu anapogusa mpira wa kwanza anakuwa ameshafanya maamuzi katika njia tatu apige pasi mbele, nyuma au aondoke na mpira. “Ana kiwango bora na maarifa mengi ana uwezo binafsi na mwepesi kucheza na wenzake pale anagundua maadui wamemzonga na anaona yeye hana uwezo wa kupanda,” anasema Kashasha.

Chanzo: mwananchi.co.tz