Manzini. Simba hawakukosea kusajili kikosi cha mauaji kimataifa na ndivyo ilivyokuwa kwa wachezaji wake, Cletous Chama, Meddie Kagere akiunganisha nguvu na Emmanuel Okwi na John Bocco waliokuwepo.
Iko hivi. Wachezaji hao, Chama na Kagere, mchezo wa kwanza waliwafunga bao moja kila mmoja na jana wakaifungia tena Simba ikishinda mabao 4-0 katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows kwenye Uwanja wa Somhlolo.
Kati ya mabao manne, Chama alifunga mawili wakati Kagere moja huku jingine likifungwa na Okwi.
Mchezo wa kwanza Simba ilishinda mabao 4-1, kwenye Uwanja wa Taifa, hivyo Simba inaingia hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao 8-1 na sasa inasubiri mshindi wa mchezo kati ya Nkana Red Devils ya Zambia na UD Songo ya Msumbiji zinazorudiana leo mjini Lusaka. Hata hivyo, katika mchezo wa kwanza uliochezwa Novemba 28 ikiwa ugenini Nkana ilishinda mabao 2-1.
Mechi za raundi ya kwanza zitachezwa kati ya Desemba 15 na 16 na marudiano ni kati ya Desemba 27 na 28.
Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na Chama kiungo kutoka Zambia, dakika ya 28 baada ya kumfinya beki wa Mbabane kisha kumchambua kipa na dakika ya 33 akaongeza la pili, mabao yaliyodumu hadi mapumziko.
Kocha wa Mbabane, Kinnah Phiri ambaye alitamba kuiua Simba, alifanya mabadiliko ya mapema dakika ya 37 kwa kuwatoa beki, Sifiso Mabila na kumuingiza mshambuliaji Tarawallie Sallieu na dakika ya 39 akamtoa kiungo mshambuliaji Richard Mccreesh na kuingia Colani Sikhondze, ambayo hayakusaidia.
Simba ilikianza kipindi cha pili kwa kujiamini na dakika ya 54, Emmanuel Okwi aliifungia bao la tatu, baada ya kuwalamba chenga wachezaji wa Mbabane kuanzia katikati ya Uwanja akiwaunga tela hadi kuujaza mpira wavuni.
Bao hilo ndilo lililowakatisha tamaa wenyeji walioonekana kuanza kulaumiana ndani na hata kwa upande wa mashabiki huku wengine wakiondoka uwanjani.
Mshambuliaji nyota kutoka Rwanda, Meddie Kagere ambaye alifunga bao la tatu mchezo wa kwanza, hakukubali kutoka uwanjani kapa bali alihitimisha karamu ya mabao alipoifungia Simba bao la nne katika dakika ya 64 kwa kuwazidi maarifa mabeki wa timu hiyo.
Endapo Simba itakutana na Nkana itabidi ijipange kwani Nkana baada ya kutinga hatua ya makundi msimu uliopita msimu huu imepania kurejea mafanikio hayo na kufanya makubwa zaidi.
Nkana iliyomaliza Ligi Kuu ya Zambia msimu huu katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 76 nne chini ya mabingwa Zesco United, imefanya vyema katika mechi zake kumi za mwisho. Ukiondoa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya UD Songo katika Ligi ya Mabingwa Afrika, katika Ligi Kuu ya Zambia, Nkana imeshinda michezo saba mitatu ikiwa ugenini na kutoka sare tatu. Aidha kwa upande wa UD Songo, kwa sasa ndiyo inayoongoza Ligi Kuu Msumbiji ikiwa imecheza michezo 13 kushinda tisa, imetoka sare mechi nne haijapoteza na ina pointi 31.
Timu hiyo ina mabao ya kufunga 14 na kufungwa moja. Pia Mtibwa Sugar jana ilishinda bao 1-0 dhidi ya Northen Dynamo ya Shelisheli. Nayo Zimamoto iliichapa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mabao 2-1.