Klabu ya soka ya Arsenal imethibitisha kuwa wamemuacha rasmi kiungo wao Santi Cazorla.
Arsenal wamethibitisha hilo kupitia taarifa waliyoitoa kwenye tovuti yao ikisema mchezaji huyo anaondoka baada ya mkataba wake kufikia mwisho.
Cazorla alijiunga na Arsenal 2012 akitokea Malaga ya Hispania. Amefanikiwa kucheza jumla ya mechi 180 akiwa na Arsenal na kufunga magoli 29 katika mashindano yote.
Pia katika misimu yake hiyo sita ndani ya timu hiyo, ameisaidia kushinda mataji mawili ya kombe la FA na mawili ya ngao ya jamii. Akiongea na tofuti hiyo ya Arsenal Mkurugenzi Mkuu wa timu hiyo, Ivan Gazidis’ amesema Cazorla ni mmoja kati ya wachezaji anaowapenda sana kuwatazama akicheza lakini pia amemshukuru kwa mchango wake alioutoa kwenye timu hiyo kwa kipindi chote hiko.
“Santi ni mmoja kati ya wachezaji wangu naopenda kuwaangalia. Uwezo wake wa asili wa miguu yote, kasi yake ya mawazo na harakati zilikuwa muhimu kwa maonyesho yetu bora katika miaka ya hivi karibuni. Anacheza na furaha na uhuru ambao ni nadra sana. Tunamtakia kila la kheri kwa siku zijazo na tunamshukuru kwa mchango wake muhimu kwa klabu yetu,” amesema Mkurugenzi huyo.
mechi ya mwisho ya Cazorla kuitumikia Arsenal ilikuwa ni Oktoba 19, 2016 wakati walipoifunga Ludogorets 6-0.