Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Cabaye, muuza korosho anayetesa pale Azam FC

74017 Cabaye+pic

Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kiungo wa Azam, Abdallah Masoud ‘Cabaye’ ni kati ya wachezaji wa Kitanzania waliopitia mazingira magumu (msoto) ya kimaisha kabla ya kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa.

Nyota huyo ambaye alianza kutamba msimu uliopita akiwa na KMC, anasema kutokana na changamoto ya ugumu wa maisha iliyokuwa kwenye familia yake ilibidi ajiingize kwenye biashara ya kuuza korosho ili apate pesa ya kununua viatu.

Akiwa kwao Mtwara, Cabaye ambaye ni kiungo mkabaji, anasema alikuwa akidamka kila siku alfajiri na kuwahi kwenye mashamba ya watu wa mikorosho kuokota korosho kabla ya kwenda shule.

“Nimefanya kazi hiyo kwa miaka mingi na ilikuwa ikinisaidia kwa sababu nilikuwa nikipata vifaa vyote vya michezo kuanzia viatu, soksi, jezi na vinginevyo. Nyumbani isingekuwa rahisi kutokana na hali ya kimaisha watoe pesa waninunulie vifaa hivyo.

“Korosho zilikuwa zikifanya mambo kwangu kuwa mepesi, nilijikuta nikianza kujihudumia nikiwa na umri mdogo na muda mwingine mambo yalipokuwa hayaendi sawa nyumbani, nilikuwa nikiokoa jahazi,” anasema.

Cabaye anasema alianza rasmi safari yake ya kucheza soka 2012 kwenye kituo cha Mtwara. Akiwa hapo alikutana na changamoto nyingi ikiwemo kuzomewa pindi anapocheza vibaya.

Pia Soma

Advertisement   ?
Kiungo huyo anasema kila alipokuwa anazomewa alikuwa akiumiza kichwa ni kwa namna gani anaweza kuwa kipenzi cha mashabiki hao ambao asilimia kubwa walikuwa watu wasiokuwa na uelewa mkubwa kuhusu soka.

“Kuzomewa kuliniumiza na niliona njia pekee ni kujiimarisha kwa kuwa fiti ili nicheze vizuri kwenye kila mchezo. Hilo lilinisaidia kuwa bora na mwishowe nikapata nafasi ya kujiunga na akademi ya Azam,” anasema.

Akiwa Azam, Cabaye anasema alijifunza mengi na kukabiliana na changamoto nyingi lakini alijipa moyo kuwa ipo siku anaweza kuwa mchezaji wa kulipwa ambaye ataisaidia familia yake kupitia kiasi atakachokuwa akikipata.

Msimu uliopita wa 2018/19, Cabaye alikuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Azam na hapo ndipo ndoto yake ilipotimia na kuanza maandalizi ya msimu huo huku akiwa na matumaini kwamba utakuwa msimu wake lakini mambo yalienda tofauti.

“Sikupata nafasi ya kutosha ndipo nilipoona kuna umuhimu wa kwenda kwa mkopo KMC ambako niliona naweza kupata nafasi ya kucheza,” anasema.

Cabaye mwenye umri wa miaka 20, anasema alikuwa na maisha mazuri KMC ambako aliichezea zaidi ya nusu ya mechi za duru la pili la Ligi Kuu Tanzania na aliifungia timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni mabao matano.

“Kocha Ettiene Ndayiragije alituamini vijana ndio maana ilikuwa rahisi kufanya maajabu na kumaliza kati ya timu nne za juu katika msimamo,” anasema.

Kinda huyo, anasema baada ya muda wake wa kuichezea kwa mkopo KMC kumalizika, alirejea Azam ambako kwa bahati nzuri ameungana tena na aliyekuwa kocha wake wa KMC, Ndayiragije ambaye amepewa mikoba ya Azam.

Furaha yangu ilikuwa kubwa kwa sababu nilipata tena nafasi ya kufanya kazi naye, kwani kwa kiasi kikubwa amechangia kunifanya nifahamike na watu waone uwezo wangu tukiwa KMC

“Alipokuja na kunikuta nimesharejea Azam alitaka tuendelee kufanya naye kazi na naamini tunaweza kufika naye mbali kwa sababu analijua vilivyo soka la Tanzania,” anasema.

Cabaye anasema ndoto zake ni kucheza soka la kulipwa na kuyafikia mafanikio ya Mbwana Samatta ambaye alitamba kwenye soka la Afrika akiwa na TP Mazembe na hatimaye kwa sasa anafanya vizuri Ulaya akiwa na KRC Genk ya Ubelgiji.

Kiungo huyo, alikuwa sehemu ya kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kilichocheza mchezo wa kwanza, Julai 28 uwanja wa Taifa dhidi ya Kenya wa kuwania nafasi ya kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezani wa ndani (CHAN).

Chanzo: mwananchi.co.tz