Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CAF yatia mkono mechi ya Simba na Yanga, Bodi ya Ligi yafunguka

85690 Pic+simba+yanga CAF yatia mkono mechi ya Simba na Yanga, Bodi ya Ligi yafunguka

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. HUKU mashabiki wa soka wakiwa hawana hakika kama pambano la kwanza la watani wa jadi, Simba na Yanga litapigwa Januari 4 mwakani kutokana na uwepo wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2020, nao Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wamewatibulia mapemaa.

Ipo hivi. Mabadiliko ya ratiba yaliyofanywa na CAF yanauweka rehani mchezo wa marudiano wa watani hao wa jadi wa soka nchini uliopangwa kuchezwa Aprili, 18 mwakani, wakati ule wa kwanza tu mpaka sasa bado haijaeleweka kutokana na kuingiliana na Kombe la Mapinduzi. Kamati ya Utendaji ya Caf, juzi Ijumaa ilitoa kalenda mpya ya mashindano na miongoni mwa mabadiliko yaliyofanyika ni kusogeza mbele Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2020 kutoka Februari hadi Aprili mwakani. Tanzania ni kati ya timu zilizofuzu fainali hizo zitakazofanyika Cameroon kuanzia Aprili 4-25, kipindi ambacho kutakuwa na mechi za raundi sita za duru la pili za Ligi Kuu Bara ukiwemo huo wa Yanga na Simba uliopangwa kupigwa Uwanja wa Taifa. Kwa ratiba hiyo mpya ya mashindano ya CAF ni wazi mchezo huo wa watani na mingine kulazimishwa kurudishwa nyuma basi kusogezwa mbele, jambo ambalo klabu zinapaswa kujiandaa kisaikolojia kukabiliana nalo. Kutokana na ufinyu wa muda na uwepo wa mashindano mengine kama vile, Kombe la Azam Sports Federation, Mapinduzi na SportPesa Super Cup ni wazi mechi hizo za ligi ambazo zimepangwa kuchezwa katika kipindi ambacho Fainali za Chan zitachezwa, zitalazimika kusogezwa mbele. Huenda hilo likapelekea kuchelewa kumalizika kwa msimu huu kwani kabla hata ya ratiba hiyo, tayari kuna timu zina viporo mkononi ambazo hazijachapangiwa tarehe ya kuchezwa, pia kuna uwezekano wa uwepo wa kambi ya Stars kujiandaa na fainali hizo za Chan 2020.

MNGUTO AFAFANUA Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB) Steven Mnguto alisema wameyapokea mabadiliko hayo ya Caf na wanayafanyia kazi. “Niwatoe wasiwasi tu kwa kuwaambia Bodi tumeshajulishwa na tumepanga kukutana na kufanya marekebisho ya ratiba yetu na baada ya hapo tutawatangazia kama mechi hizo zitasogezwa mbele au zitarudishwa nyuma,” alisema Mnguto na kuongeza; “Sisi wenyewe tulikuwa tunasubiria Caf watoe ratiba ya Chan ili tuone tunajipanga vipi hivyo baada ya kujua mashindano hayo yanaanza lini, nadhani ni wakati sasa wa kulifanyia kazi hilo.” Ofisa Mtendaji wa KMC, Walter Harrison alishauri TPLB kutengeneza ratiba rafiki ambayo haitaziumiza klabu. “Kwanza ni wakati sahihi kwa Bodi ya Ligi kujipanga mapema baada ya Caf kutoa ratiba hiyo ili kuzinusuru klabu kwa sababu hadi sasa kumekuwa na mabadiliko mengi ya ghafla ambayo yanaziacha timu katika wakati mgumu,” alisema Harrison na kuongeza; “Bodi ya Ligi wanatakiwa waangalie wanasaidia vipi klabu kwa sababu kwa hali ilivyo ya haya mabadiliko ya mara kwa mara na ya ghafla, hatuwezi kupata ule ushindani ambao utatupatia bingwa atakeymudu ushindani wa kimataifa.” Harrison alisema kwa mfano mchezo wao dhidi ya Mbao waliambiwa ungechezwa baada ya mapumziko ya Kombe la Chalenji na kuwapa ruksa wachezaji, lakini ghafla mashindano hayo yamesogezwa mbele na ndani ya muda mfupi tunajulishwa wana mechi dhidi ya Yanga na tayari baadhi ya wachezaji  wameshaenda makwao kwa mapumziko.

Chanzo: mwananchi.co.tz