Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

CAF yaibeba Yanga Ligi ya Mabingwa, KMC ndani kimataifa

61335 Pic+yanga+cuf

Tue, 4 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limeibeba Yanga kushiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao baada ya kuongeza idadi ya timu kutoka mbili hadi nne kwa Tanzania kushiriki mashindano ya kimataifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema CAF imeongeza idadi ya timu za Tanzania zitakazoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Taarifa hiyo ya TFF iliyosainiwa na Ofisa Habari wa Shirikisho hilo, Clifford Ndimbo ilieleza Tanzania imejiongezea nafasi ya kupeleka timu zake katika Mashindano ya Afrika baada ya Tanzania kuwa katika nafasi 12 bora kwenye viwango vya CAF.

"Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu zilizofanyiwa marekebisho na kamati ya Utendaji baada ya kupatikana  nafasi nne (4) timu za Tanzania zitakazowakilisha kwenye mashindano hayo  ni Simba, Yanga (CAF CL), Azam Fc na KMC kombe la Shirikisho (CAF CC).

Taarifa hiyo ilieleza KMC atawakilisha Kombe la Shirikisho kwa mujibu wa kanuni hiyo ambayo inatamka kama timu iliyomaliza nafasi tatu itakuwa ndio bingwa wa Kombe la Fa basi mshindi wa nne anapata nafasi ya kucheza kombe la shirikisho kwa sababu bingwa wa Fa anaiwakilisha nchi kwenye mashindano hayo.

Kuongezwa kwa timu hizo imekuwa habari njema kwa Yanga iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu msimu huu hivyo sasa wanapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya klabu barani Afrika.

Pia Soma

KMC iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya kwanza nayo imepata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na Azam FC.

CAF yafungua pazia la usajili

Tayari CAF imefungua dirisha kwa mashindano kusajili timu kupitia mtandao wa CMS, huku mwisho wa usajili ni Juni 30, 2019 ambapo TFF inatakiwa iwe imesajili timu zitakazoshiriki kwenye mashindano ya kimataifa msimu wa 2019/20.

Rais wa TFF, Wallace Karia amezitaka klabu zilizopata nafasi kusajili kwa umakini na kujiandaa kwa mashindano ya CAF ili kutopoteza nafasi ya kuingiza timu nne katika mashindano haya.

Chanzo: mwananchi.co.tz