Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bosi GSM amchangia Mdamu Tsh. Milioni 6 za matibabu

Gsm Pc Data Bosi GSM amchangia Mdamu Tsh. Milioni 6 za matibabu

Thu, 26 Aug 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

MFANYABIASHARA na bilionea Ghalib Said Mohamed, ambaye pia ni Rais wa Kampuni ya GSM ametoa Shilingi 6 Milioni kama mchango wake kwa ajili ya matibabu ya mchezaji wa Polis Tanzania Gerard Mathias Mdamu.

Gerard Mathias Mdamu alivunjika miguu yote miwili Julai 9, wakati kikosi cha timu ya Polis Tanzania kikitoka mazoezini katika Uwanja wa TPC Mkoani Moshi wakielekea kambini kwa ajili ya kumalizia mechi za mwisho za msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu usliomalizika 2020/2021.

Nyota huyo amelazwa Hospitali ya Taifa kitengo cha mifupa (Moi) baada ya kupata ajali ya gari akiwa na wenzake wakitoka mazoezini walipokuwa wakijiandaa kumaliza mechi za msimu uliopita.

Wakati akifanya mahojiano na kipindi cha Sport Arena Wasafi FM, msemaji mpya wa Yanga Haji Manara amesema Ghalib ameguswa na tukio hilo la Gerard kupata majeraha hivyo kuamua kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kitamsaidia katika matibabu yake.

"Ghalib ni mtu wa watu na kama wengine walivyojitokeza kumchangia mchezaji huyo wa Polisi Tanzania nae pia ameguswa na kutoa mchango wake ambapo tutaukabidhi sehemu husika," alisema Manara.

Naye Haji Manara kwa upande wake amechangia kiasi cha dolla za kimarekani 300$ na sh10,000 ya kitanzania kwa ujumla ni sh700,000 kwa ajili ya matibabu ya mchezaji huyo.

"Natoa laki saba ambayo ni mshahara wangu wa mwezi wa saba kama sehemu ya kumchangia Mdamu ambaye sote kwa ujumla tunajua hali anayopitia," alisema Manara.

Katika hatua nyingine Manara alisema wao kama viongozi wa Yanga wataendelea kumchangia Mdamu ili kuhakikisha anapona na kurejea katika hali yake ya kawaida.

"Huu ni mwanzo tu ila malengo yetu kama Yanga kwa ujumla ni kumsaidia Mdamu kupata matibabu zaidi ili tumuone akirejea kwenye majukumu yake ya kila siku kama walivyo watu wengine," alisema.

Wadau mbalimbali wa michezo nchini wamekuwa wakiguswa na kuamua kumchangia Mchezaji huyo huku wengi wao wakiandaa mechi za hisani ili tu kuhakikisha wanapata fedha ambayo itamsaidia katika matibabu yake.

Mdamu anaendelea kupatiwa matibabu ambapo leo anatarajiwa kufanyiwa operesheni kwenye miguu yake yote miwili iliyovunjika.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz