Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bodi ya Ligi yajitetea mabadiliko ya ratiba

11822 Pic+bodi TanzaniaWeb

Tue, 14 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Changamoto ya viwanja imeendelea kuwa chanzo cha kupanguliwa kwa ratiba ya Ligi Kuu baada ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutangaza mabadiliko mengine ya ratiba ya ligi hiyo kabla hata haijaanza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ligi Kuu, Boniface Wambura alisema sababu ya kubadili ratiba ya mechi hizo za Simba ni kutokana na Uwanja wa Taifa kutumika kwa mechi za mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

“Tumepata barua kutoka Wizara inayomiliki Uwanja wa Taifa kuwa uwanja huo hautoruhusiwa kutumika tena kuanzia tarehe 22 Agosti hadi Septemba Mosi, Vilevile tumepokea barua kutoka kwa wamiliki wa Uwanja wa Jamhuri Morogoro kwamba uwanja umekodiwa kwa ajili ya shughuli za kijamii kuanzia Agosti 23 hadi 30,” alisema na kuongeza.

“Kwa hiyo hizo mechi ambazo tulikuwa tumeziweka hapo tunalazimika kuziondoa na uamuzi ni kwamba tutazihamishia Uwanja wa Uhuru. Tarehe zitabaki kama zilivyo isipokuwa kwa mechi moja,” alisema Wambura.

Mabadiliko hayo ya ratiba ya Ligi ambayo yatahusu mechi zitakahusisha timu za Yanga, Simba, Prisons, Mbeya City na Lipuli kwa mara nyingine yametokana na muingiliano wa matukio tofauti yanayofanyika kwenye viwanja vilivyopaswa kuchezwa mechi hizo.

Simba ambayo itakuwa ikitetea ubingwa wa Ligi Kuu itaathirika zaidi na mabadiliko hayo kutokana na mechi zake tatu za mwanzo kuhamishwa kutoka kwenye uwanja uliopangwa kwenye ratiba ya awali.

Mchezo wa ufunguzi uliopangwa kuchezwa Agosti 22 kwenye uwanja wa Taifa baina ya Simba na Prisons umehamishiwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini ingawa utachezwa siku hiyo, mabadiliko ambayo yamegusa pia michezo mingine ya timu hiyo dhidi ya Mbeya City na Lipuli. Simba italazimika kucheza mchezo wake na Mbeya City, Agosti 25 kwenye uwanja wa Uhuru badala ya Uwanja wa Taifa lakini pia mechi yake ya Septemba Mosi dhidi ya Lipuli iliyotakiwa kuchezwa Uwanja wa Taifa nayo imepelekwa Uwanja wa Uhuru, ukisogezwa mbele kwa siku moja hadi Septemba 2.

Mechi ambayo ilitakiwa kuchezwa Septemba Mosi kati ya Simba na Lipuli wenyewe umesogezwa mbele kwa siku moja hadi Septemba 2 na utachezwa kwenye uwanja wa Uhuru,” alisema Wambura.

Mchezo ambao Yanga ingecheza ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, Agosti 23 umerudishwa kwenye Uwanja wa Uhuru jijini kutokana na kuwepo kwa shughuli nyingine kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, ambao ulipangwa kutunika kwa mechi hiyo.

Kutokana na mabadiliko hayo wadau mbali mbali wamezungumzia hilo, Kocha wa zamani wa Bandari Mtwara na Yanga, Kennedy Mwaisabula ‘Mzazi’ alisema tatizo la klabu nyingi kutokuwa na viwanja, limekuwa likichangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko yasiyo ya lazima ya ratiba za mechi za ligi. “Ikumbukwe kuwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu nyingi za ligi hazina viwanja. Viwanja vina wamiliki wake ambao huwezi kuwapangia matumizi yake,” alisema Mwaisabula.

Katika hatua nyingine, Wambura alisita kuzungumzia suala la hatima ya mdhamini mkuu wa Ligi Kuu msimu huu, akisema hilo litajulikana leo.

Chanzo: mwananchi.co.tz