Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco turufu ya Stars AFCON

49347 Bocco+pic

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Shujaa wa Tanzania kuelekea kwenye fainali za Afrika (Afcon) 2019, John Bocco, ni karata ya turufu na taifa litajivunia kumshawishi afute mpango wa kujiuzulu aliokuwa nao mwaka 2012, makocha wamesema.

Makocha mbalimbali wamezungumzia kuzaliwa upya kwa Bocco na kuafiki kwamba hawajui ingekuwaje kama asingefuta uamuzi wake wa kustaafu.

Kocha wa zamani wa Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla amesema Bocco amebadilika sana kiuchezaji na nafasi aliyopangwa Jumapili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Uganda ‘The Cranes’, inamfaa kwani inampa uhuru wa kucheza mpira na kufanya maamuzi mazuri.

“Kuanzia mechi na AS Vita akiwa na klabu yake Simba na hii ya timu ya Taifa dhidi ya Uganda, Bocco alinishangaza sana kiwango chake, yaani alikuwa yuko vizuri sana kiuchezaji na anajitolea kwa asilimia 100.

“Faida ya kucheza pembeni kwanza unakuwa na eneo kubwa la kujidai yaani ukipata viungo wazuri wanaokupa pasi nzuri ukimtoka mchezaji mmoja tu wa timu pinzani una uhakika wa kupiga krosi.

“Lakini ukicheza mshambuliaji wa kati ukipewa pasi kuna wachezaji watatu wa upinzani wanakusubiri mgongoni. Kwa hiyo nafasi aliyopangwa ilimpa nafasi atanue uwanja na kucheza kwa uhuru lakini pia ameonyesha dhamira ya kujituma na sio tena Bocco wa zamani,” alisema Dk Msolla.

Naye kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula amesema Bocco ni mmoja kati ya washambuliaji wazuri nchini licha ya mashabiki wakati mwingine kumbeza.

“Licha ya mechi ile kuchezeshwa kama winga nafasi ambayo huwa hachezi mara nyingi, alionyesha kuwa yeye ni mpambanaji, alicheza vizuri sana na kutoa pasi mbili za mabao.

“Sasa hivi amejitambua na kuona kuwa kama anashindwa kufunga basi asababishe bao na ndicho anachokifanya, hivyo hata wale waliokuwa wanambeza sasa hivi amewanyamazisha,” alisema Mwaisabula.

Mshambuliaji huyo aliyepiga soka la kiwango cha nyota wa mchezo, alitoa ‘asisti’ zilizozaa magoli mawili katika ushindi wa 3-0 wa Stars dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili iliyopita, lakini pengine matokeo yangekuwa tofauti kama angesimamia uamuzi wake ya kujiuzulu kuitumikia timu hiyo.

Siku moja Machi 2012, Bocco aliandika barua kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulitaarifu kuhusu uamuzi wake wa kustaaafu kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania ’Taifa Stars’.

Nyota huyo ambaye wiki mbili zilizopita aliisaidia pia klabu yake ya Simba kutinga robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kutoa ‘asisti’ ya bao lililowavusha, katika barua yake ya kujiuzulu wakati huo alieleza kutofurahishwa na tabia za mashabiki kumzomea kila alipopangwa.

Bocco alikaririwa katika barua hiyo kuwa alifikia uamuzi hayo baada ya kufikiria sana.

Wakati huo, straika huyo mwenye mwili mkubwa, alikuwa akiichezea Azam na ilisemekana kwamba ‘tabia’ yake ya kuzitungua timu za Simba na Yanga kila alipokutana nazo ilichangia kuandamwa kwake kwenye timu ya Taifa.

Ni miaka saba sasa tangu Bocco ajiuzulu kabla ya kushawishiwa na kurejea kikosini na mashabiki wameanza kumuelewa na wanaimba jina lake majukwaani. Bocco amesema anajisikia fahari kuvaa jezi ya timu ya taifa na anayoyafanya uwanjani ni uthibitisho.

Alisema atafurahi kama atakuwa mmoja swa watakaoenda kuipigania bendera ya Tanzania nchini Misri katika fainali ambazo Stars itashiriki kwa mara ya pili baada ya miaka 39 ya kuhangaika.



Chanzo: mwananchi.co.tz