Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco kuikosa Yanga, Simba yatakata

19070 Pic+bocco TanzaniaWeb

Tue, 25 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Shinyanga, Mwanza. Furaha ya mabao mawili aliyoifungia Simba dhidi ya Mwadui, ilimalizika kuwa kilio kwa nahodha John Bocco, baada ya kuonyeshwa kadi nyekundu itakayomfanya akose mechi ya watani wa jadi dhidi ya Yanga, Septemba 30 jijini.

Bocco alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 81 na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro, baada ya kumpiga ngumi ya kisogo beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga.

Awali, Mgunga alimchezea madhambi mshambuliaji huyo nguli, alipokuwa kwenye harakati ya kuokoa shambulizi lililokuwa linaelekezwa langoni mwake.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu, Bocco atakosa mechi tatu zinazofuata ikiwemo dhidi ya Yanga na huenda adhabu hiyo ikaongezeka kutokana na kosa alilofanya kuwa sio la kiungwana.

Msimu uliopita Mgunga ndiye aliyemchezea madhambi Bocco katika mechi ya mzunguko wa kwanza na kumsababishia majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja muda mrefu.

Mechi ya jana ilitawaliwa na matukio yasiyofurahisha na yanayovutia kwa Bocco kwa kuwa mbali na kadi hiyo nyekundu, mabao yake mawili yalitoa mchango mkubwa kwa Simba kushusha presha baada ya kushindwa kupata ushindi katika michezo miwili mfululizo dhidi ya Ndanda na Mbao FC ambapo ilipata pointi nne, ikifungwa moja na kutoka sare moja.

Bocco amefikisha jumla ya mabao 100 katika Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo amefunga katika timu mbili tofauti Azam na Simba.

Hata hivyo, kadi nyekundu ya Bocco haikuweza kuizuia Simba kuibuka na ushindi mnono wa ugenini wa mabao 3-1 ambao umeifanya kufikisha pointi 10 na kusogea hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kabla ya mchezo wa jana usiku baina ya Yanga na Singida United.

Vijana wa kocha Patrick Aussems walipeleka mashambulizi mara kwa mara langoni mwa wapinzani wao huku wakitawala mchezo kwa kupigiana pasi nyingi ingawa safu ya ulinzi ya Mwadui ilikuwa imara kuokoa hatari zilizoelekezwa langoni mwao.

Tofauti na mchezo uliopita dhidi ya Mbao ambao safu ya ulinzi ya Simba ilifanya uzembe uliochangia wapinzani wao kupata bao pekee lililowafanya wapoteze mechi hiyo, jana mabeki wa timu hiyo walicheza kwa nidhamu huku wakimlinda vyema kipa Aishi Manula.

Wakati wengi wakiamini mechi hiyo ingekwenda mapumziko timu hizo zikiwa hazijafungana, Bocco aliipatia Simba bao la kuongoza dakika ya 41 kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa baada ya beki Miraji Maka kumfanyia madhambi Shiza Kichuya ndani ya eneo la hatari alipokuwa akiwahi pasi ya kiungo Cletus Chama.

Kabla hata Mwadui hawajamaliza kujiuliza bao hilo, dakika nne baadaye Bocco aliipatia Simba bao la pili akimalizia vyema mpira wa krosi ya Meddie Kagere uliompita kipa Arnord Massawe.

Dakika moja baada ya filimbi ya kuashiria kuanza nusu ya pili ya mchezo, Kagere aliipatia Simba bao la tatu akitumia uwezo binafsi wa kuiwahi pasi ndefu ya Kichuya aliyemtoka beki wa Mwadui kabla ya kuachia kiki kali iliyomshinda Massawe na kujaa kimiani.

Licha ya kufungwa, Mwadui ilikuja kivingine dakika 45 za kipindi cha pili kwa kushambulia lango la Simba jambo lililochangia wachezaji wa timu zote kuchezeana ubabe na kumlazimisha mwamuzi Vitalis kutoa kadi kwa pande zote mbili.

Miraji Maka, Erasto Nyoni na Charles Ilanfya walionywa kwa kadi za njano kutokana na utovu wa nidhamu. Pengo la Bocco liliinufaisha Mwadui baada ya kupata bao dakika ya 89 kupitia kwa Ilanfya aliyefunga kwa kubetua mpira mrefu aliopigiwa mbele ya beki Pascal Wawa.

Timu zote mbili zilifanya mabadiliko Simba ilimtoa Kichuya na kumuingiza Mohammed Ibrahim, Mwadui ikimtoa Innocent Edwin na kuingia John Kasanzu. Matokeo mengine mkoani Mwanza bao la kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu la dakika ya 59 lilitosha kuizamisha Alliance nyumbani kwa kipigo cha 1-0 dhidi ya Azam. Mbeya City ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar. lilifungwa na Eliud Ambokile dakika ya 34 na lile la kusawazisha la Kagera Sugar lilifungwa na Selemani Mangoma dakika ya 52.

Chanzo: mwananchi.co.tz