Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco, Kagere waipa jeuri

49695 BOCCO+PIC

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MASTAA watatu tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Simba wataukosa mchezo wa leo Jumapili dhidi ya Mbao FC, lakini uwepo wa nahodha John Bocco na Meddie Kagere unawapa jeuri mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, kulipa kisasi wakati timu hizo zitakapokutana Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Kagere na Bocco wameunda safu kali ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikizitesa timu pinzania msimu huu na uwepo wao bila shaka unawapunguzia presha Simba ambao watawakosa Emmanuel Okwi, Cletous Chama na Jonas Mkude waliochelewa kujiunga kikosini baada ya kumaliza majukumu ya timu zao za taifa.

Bocco amekuwa kwenye kiwango bora siku za hivi karibuni katika ufungaji na upikaji wa mabao na uelewano wake na Kagere, ambaye amekuwa akitumia vyema nafasi anazopata ndani ya eneo la hatari kufumania nyavu, kunawapa imani kubwa Simba ya kuondoka na ushindi licha ya kuwakosa nyota hao.

Ubora wa Bocco ulijidhihirisha Jumapili iliyopita na alikuwa chachu ya ushindi wa mabao 3-0 ambao iliupata timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ilipocheza na Uganda kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Kana kwamba haitoshi ni Bocco, ambaye alipiga pasi za mwisho kwenye mabao ya ushindi ambayo Simba ilipata dhidi ya AS Vita, Yanga na Al Ahly huku pia akiwa amefunga mabao tisa kwenye ligi msimu huu.

Lakini, Kagere ndiye amekuwa kinara wa ufungaji kwenye kikosi cha Simba msimu huu kwani akipachika mabao 12, pia ana mabao sita Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo timu hiyo imetinga hatua ya robo fainali. Kasi na ubora wa Simba na wachezaji wake unawaweka kwenye hali nzuri kisaikolojia ambayo itawafanya wawe na asilimia kubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Mbao FC ambayo imekuwa ikiwasumbua mara kwa mara pindi wanapokutana.

Wakati Mzamiru Yassin akitarajiwa kuziba pengo la Mkude, Hassan Dilunga huenda akasimama mahali pa Chama huku nafasi ya Okwi ikitarajiwa kuchezwa na Haruna Niyonzima.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alikiri kukosekana kwa wachezaji hao ambako kumetokana na sababu tofauti.

“Okwi ana matatizo ya kifamilia na ugonjwa, Mkude anatakiwa kuingia leo (jana) nae alikuwa na matatizo binafsi na Chama anarudi leo toka Zambia alikoenda kwenye timu ya taifa,” alisema Rweyemamu.

Hata hivyo, alisema pamoja na kuwakosa wachezaji hao watatu muhimu, kikosi cha Simba kimejiandaa vizuri kuhakikisha kinapata ushindi kwenye mchezo huo ingawa wanaipa heshima Mbao FC.

“Ukiondoa hao, wengine waliobakia wako vizuri na wazima wa afya na kila mmoja yuko tayari kucheza iwapo benchi la ufundi litampa nafasi.

Kimsingi tunaamini mechi itakuwa nzuri na mashabiki wategemee kuona kiwango bora kutoka kwa kila timu na yule ambaye amejiandaa vizuri zaidi tunaamini ndiye atapata matokeo,” alisema.

Mbali na hilo, Simba pia huenda wakanufaika kukutana na Mbao ambayo inahaha kurejea katika hali yake ya kawaida baada ya kupita kipindi kigumu cha kupoteza ubora na ufanisi wao pamoja na migogoro baina ya wachezaji na benchi la ufundi.

Changamoto hizo zimeifanya Mbao FC kupoteza michezo yake mitatu mfululizo iliyopita dhidi ya Yanga waliyofungwa nyumbani mabao 2-1, wakafungwa bao 1-0 na Lipuli huku pia wakifungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo yasiyoridhisha ndio yalipelekea Mbao FC kumtimua kocha wake mkuu, Ally Bushiri na kumuajiri Salum Mayanga, ambaye ameongezewa nguvu kwa kuletewa msaidizi wake, Fulgence Novatus.

Rekodi za michezo iliyopita nyuma ambayo imekutanisha timu hizo, zinaweza kuwa chachu ya ushindani mkubwa ndani ya uwanja baina ya timu hizo kama ambavyo imezoeleka pindi zikutanapo.

Kabla ya mchezo wa leo, Simba na Mbao zimekutana mara saba na Simba imeshinda mara tano, kutoka sare moja na kupoteza moja. Hata hivyo mara nyingi ushindi wa Simba katika mechi hizo umekuwa ukipatikana kwa ugumu.

Ushindi dhidi ha Mbao utaifanya Simba ifikishe pointi 57 ambazo zitaifanya iwe nyuma ya kinara Yanga kwa pointi 10 na kama hapo baadaye itaweza kuibuka na ushindi kwenye mechi zake zote za viporo ilizobakiza ili iwe sawa na Yanga, itakuwa kileleni mwa msimamo wa ligi na pointi 75 ambazo zitakuwa nane zaidi ya zile za watani wao.

Kwa upande wa Mbao wenyewe matokeo ya ushindi angalau yatawafanya wafikishe pointi 39 ambazo zitawaondoa kwenye nafasi ya 14 hadi ya nane kwenye msimamo wa ligi.

Pamoja na kuwa nafasi ya 14, Mbao hawako salama sana hivyo ni wazi mchezo huo utakuwa na ushindani kwani wanaizidi Biashara United inayoshika nafasi ya 19 kwa pointi sita tu.

Kwa kulitambua hilo, hata benchi la ufundi la Mbao linakiri linakabiliwa na presha kubwa ya mchezo huo ingawa watahakikisha wanakabiliana nayo.

SIMBA WAKARABATI UWANJA

Viongozi wa matawi ya Simba mjini hapa, waliamua kuufanyia usafi Uwanja wa Jamhuri mjini Moro baada ya uwanja huo kutofyekwa nyasi.

Meneja wa uwanja huo, John Simkoko alisema uongozi wa Simba umechagua uwanja huo kama wa nyumbani kufuatia ule wa Taifa, Dar es Salaam, kufanyiwa ukarabati kupisha matumizi ya mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17).

“Wanasimba wameamua kuondoa magugu ndani ya uwanja, kujaza vifusi sehemu zenye mashimo na kazi hiyo imefanyika kwa kipindi cha wiki tatu,” alisema Simkoko.

Mwenyekiti wa tawi la Simba la Shujaa Mjipya, Said Mkwinda alisema wameng’oa majani, kujaza vifusi, kumwagia maji majani, kufanya ukarabati mdogo kwenye vyoo, vyumba vya wachezaji na waamuzi.

“Kazi kubwa tuliyofanya kipindi cha zaidi ya wiki tatu ni hiyo, yote hii ni baada ya kuona uwanja haupo kwenye mazingira mazuri ikiwemo kuweka mfumo wa umeme wa kuvuta maji kutoka kwenye tanki la maji kwa ajili ya kumwagilia nyasi,” alisema Mkwinda.



Chanzo: mwananchi.co.tz