Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bocco, Aussems watwaa tuzo ya mwezi TFF

50322 Pic+tuzo

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba, John Bocco na kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems wametwaa tuzo ya mwezi Machi inayotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Bocco ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Donald Ngoma wa Azam FC na Jaffari Kibaya wa Mtibwa Sugar SC alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa na Kamati ya Tuzo ya TPL.

Kwa mwezi huo wa Machi, Simba ilicheza mechi tatu na kushinda zote, ambapo Bocco alitoa mchango mkubwa kwa timu yake akifunga mabao manne na kuifanya Simba iendelee kubaki nafasi ya tatu.

Kwa upande wa Ngoma alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Azam FC kwa mwezi huo, ambapo timu yake ilicheza mechi tatu ikishinda zote na kuendelea kubaki nafasi ya pili, akifunga mabao manne.

Mshambuliaji Kibaya alikuwa chachu ya mafanikio ya Mtibwa Sugar SC ambayo ilicheza mechi nne, ikishinda tatu na kupoteza moja, huku ikipaa kutoka nafasi ya 12 hadi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 20.

Kwa kuibuka mchezaji bora, Bocco atazawadiwa Sh 1,000,000 (milioni moja) na kombe (trophy) kutoka kwa wadhamini wa tuzo Biko Sports pamoja na kisimbusi kutoka Azam TV ambao ndiyo wenye haki ya matangazo ya TPL.

Aussems amechaguliwa kuwa kocha bora wa mwezi Machi akiwashinda Kocha Mkuu wa Azam, Abdul Mingange na Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila.

Aussems ameifanya Simba iendelee kung’ara katika ligi hiyo ambapo kwa mwezi huo ilishinda michezo yote mitatu iliyocheza ikiwa nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo.

Kocha huyo pia atazawadiwa Sh 1,000,000 (milioni moja) na kombe (trophy) kutoka Biko Sports.



Chanzo: mwananchi.co.tz