Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bingwa Ligi Kuu kuvuna mil 500/-

D573e14bf602a84fe8548753e6c8a0bb Bingwa Ligi Kuu kuvuna mil 500/-

Wed, 26 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na Azam Media zimesaini mkataba wa kihistoria wa udhamini wa kurusha matangazo ya Ligi Kuu Tanzania Bara wenye thamani ya Sh bilioni 225.6 kwa miaka 10, utakaomfanya bingwa wa msimu ujao kuondoka na kitika cha Sh milioni 500 kama bonasi.

Dau hilo ni kubwa ikilinganishwa na lile la miaka mitano iliyopita ambapo pande hizo mbili zilisaini mkataba kama huo wa Sh bilioni 23.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kusaini mkataba huo iliyofanyika Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema tukio hilo limekuja baada ya Azam Media kushinda zabuni waliyokuwa wameitangaza tangu Aprili 2, mwaka huu.

“Tunawapongeza Azam Media kwa kushinda zabuni, kiwango hicho cha fedha ni ukijumlisha na kodi. Haijawahi kutokea mkataba kama huu katika historia ya soka letu. Miaka ya karibuni ligi yetu imekuwa ikiimarika kwani tunashika nafasi ya nane Afrika,” alisema.

Karia alisema mkataba huo ni kwa ajili ya TV tu na kwamba wanatarajia kupata na kituo kimoja cha redio kitakachoingia udhamini nao.

Alisema ana imani kuwa udhamini huo utavutia wachezaji wengi kuja kucheza soka nchini na ushindani kuongezeka.

Rais huyo wa TFF alisema udhamini huo ni sehemu tu, kwani wanakusudia kupata wadhamini wengine kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo waliopo sasa, hivyo wanatarajia kupata fedha nyingine zaidi ya Sh bilioni 30.

“Lazima timu zioneshe matumizi kila msimu ili kupata fedha hizo. Kipaumbele muhimu kwa ajili ya fedha hizo ni kulipa wachezaji mishahara, usafiri na matibabu na sio usajili. Pia waamuzi watakuwa wanalipwa vizuri zaidi,” alisema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media, Tido Mhando alichambua fedha hizo, akisema wamekubaliana asilimia 67 ya malipo ya kila msimu ziende moja kwa moja kwa timu zinazoshiriki Ligi Kuu.

Alisema msimu wa kwanza yaani ujao wa 2021/2022, Azam Media itatoa Sh bilioni 12 huku klabu zikipata Sh bilioni 8 na sehemu ya fedha zinazobakia zitasaidia maendeleo ya soka, TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB ).

“Fedha hizi zitakuwa zikiongezeka kila msimu na msimu wa mwisho wa mkataba yaani 2030/2031, Azam Media itatoa Sh bilioni 28 na wakati huo timu zote kwa ujumla zitapata Sh bilioni 19,”alisema Mhando.

Alisema mbali na hayo, kutakuwa na bonasi kwa klabu hizo ili kufanya ligi iwe na ushindani mkubwa kwa kila nafasi ya msimamo wa ligi kila inapofikia tamati.

Mhando alifafanua kwa misimu mitatu ijayo yaani 2021/22 mpaka 2023/24, bingwa wa Ligi Kuu atapata bonsai ya Sh milioni 500 kwa msimu, mshindi wa pili Sh milioni 250, wa tatu Sh milioni 225 na nafasi ya nne Sh milioni 200.

“Fedha hizo zitakuwa zikiongezeka kila msimu na ndio maana msimu wa 2028/29 mpaka 2030/31 bingwa atakuwa akipata Sh milioni 700, wa pili Sh milioni 325, nafasi ya tatu Sh milioni 275 na ya nne Sh milioni 250,” alisema.

Alisema bonasi hizo hazitaishia kwa timu nne pekee, bali kuanzia nafasi ya tano kuanzia msimu ujao atapata Sh milioni 65, ya sita Sh milioni 60, ya saba Sh milioni 55, ya nane Sh milioni 50, ya tisa Sh milioni 45, ya 10 Sh milioni 40, ya 11 Sh milioni 35, anayefuatia hadi ya 13 watapata Sh milioni 30, 25 na 20, ambapo pia timu zinazocheza mtoano zitapata Sh milioni 20.

Alisema anatamani kuona ligi ya Tanzania inashika nafasi ya tatu Afrika na kuongeza kuwa wamekusudia kuimarisha ubora wa matangazo yao kwa kuweka miundombinu ya taa katika baadhi ya viwanja ili kuonesha mechi za usiku na kufunga mbao za kidigitali za matangazo ya biashara viwanjani.

Chanzo: www.habarileo.co.tz