Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bilionea GSM afanya kufuru Yanga

77584 GSM+PIC

Sat, 28 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ACHANA na yale maandalizi yaliyofanywa na Yanga kwa ajili ya mechi yao ya marudiano ya kesho Jumamosi kule Zambia dhidi ya Zesco United, unaambiwa bilionea wa GSM, ameendelea kufanya kufuru Jangwani kwa kipindi kifupi wale walioibeza timu hiyo wataishangilia.

Kama hujui kila mwezi Yanga ilikuwa ikipata hasara ya zaidi ya Sh 4.5 milioni kwa kukodi uwanja wa kufanyia mazoezi, lakini GSM iliyoingia mkataba na klabu hiyo imeamua kuukarabati Uwanja wa Kaunda, ikiwa na mpango wa kuyageuza makao makuu ya klabu hiyo kuwa kama hoteli ya kisasa ili kuipunguzia gharama.

Bilionea wa GSM amedhamiria kuyafanya makao ya Yanga kuwa kama ya Klabu ya Fenerbehce ya Uturuki, mpango mzima ukianza rasmi Desemba mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Yanga ukarabati wa Uwanja wa Kaunda ambao umesawazishwa kifusi unafanywa kama hisani na kampuni hiyo ikishirikiana na kamati maalumu ya klabu hiyo, lakini ikiwa pia imetenga kiasi cha Sh 150-200 milioni kwa ajili ya ukarabati wa jengo la klabu hiyo ili wachezaji wahamie hapo badala ya kuteketeza pesa hotelini.

Enzi za utawala wa Tarimba Abbas aliwahi kukarabati vyumba vya jengo hilo na wachezaji kukaa klabuni hapo, lakini alipojiuzulu tu, kila kitu kiliyeyuka.

Tuanze na hili la uwanja, Mwanaspoti limeshuhudia vifusi vikisambazwa na likajulishwa ni maandalizi ya kurejesha uwanja huo kutumika kama zamani na mipango ni kuwa na viwanja viwili, kimoja cha nyasi bandia na kingine cha asilia.

Pia Soma

Advertisement

NYASI DESEMBA

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten ameweka wazi zoezi la upandaji wa nyasi kwenye Uwanja wa Kaunda utaanza Desemba mwaka huu.

Uwanja huo utakuwa moja ya viwanja viwili vilivyo katika mipango yao kwani mbali na huo wa nyasi asili, mwingine utakuwa na nyasi bandia.

“Kwa maana hiyo wakati dirisha dogo la usajili (litaanza Novemba 15-Desemba 15) linakamilika na sisi tunaanza zoezi la upandaji wa nyasi kwenye uwanja wetu, mpango inakwenda vizuri,” alisema Ten.

Aliongeza, kuhusu eneo hawana wasiwasi kwa sababu sehemu yao ni kubwa na kwa mikakati waliyoipanga itafanikiwa bila tatizo; “Kazi iliyopo ni kuweka nguvu katika umwagaji wa vifusi.”

Ten alifafanua, ujenzi wa uwanja wao unafanyika chini ya kampuni binafsi.

“Uwanja huo wa nyasi asili hautakuwa mkubwa sana na utafanana na ule wa Azam Complex, utakaokuwa mkubwa ni wa nyasi bandia na utajengwa baada ya huo wa kwanza kukamilika,” alisema Ten.

Pia, uwanja wa nyasi asili unaofananishwa na Azam Complex utakuwa na urefu wa mita 100, wakati wa taifa ni mita 110.

Mwanaspoti lilishuhudia vifusi vikimwagwa uwanjani hapo wakati wa zoezi hilo linaendelea kusawazishwa.

Hata hivyo, harakati za kuhakikisha Yanga inakuwa na uwanja wake wa mazoezi zilianza tangu alipokuwa madarakani aliyekuwa Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa na serikali iliwahi kuzuia mipango ya kupanuliwa kwa eneo hilo kwa sababu lipo kwenye mkondo wa bahari na kipindi cha mvua hukumbwa na mafuriko, ndipo uongozi wa Mkwasa ukaja na wazi la kutanguliza vifusi.

Msikie Mtaaluma

Mtaalamu wa upandaji nyasi wa Tanzania ambaye ametengeneza viwanja tofauti nchini kama wa Simba Bunju, Sokoine Mbeya, Singida, Mtibwa na Musoma, Sidy Omary alisema, nyasi zinapopandwa hazichukui muda kukua na hutumika baada ya miezi miwili.

“Unapomwaga mbegu baada ya siku 10, zinaanza kuota. Kama ukimwaga na mbolea yale ngombe, siku tisa tu majani yanachomoza na ndivyo tulivyofanya Uwanja wa Simba. Baada ya hapo zinaanza kufyekwa kuanzia miezi miwili hadi mitatu,” alisema Sidy.

Kutokana na kauli ya Ten, kama Yanga itapandaji nyasi hizo Desemba kutokana na muda wa ukuaji wa nyasi hizo hadi Februari mwakani itaanza kuutumia uwanja wake.

KUPUNGUZIWA GHARAMA

Endapo Uwanja wa Kaunda utakamilika, Yanga itaokoa sehemu kubwa ya pesa ambazo inalipa kwenye viwanja mbalimbali vya kufanyia mazoezi.

Yanga hufanya mazoezi zaidi kwenye Uwanja wa Chuo Cha Polisi ingawa wakati mwingine hutumia Uhuru, Gymkhana na Boko Veteran ambavyo gharama yake ni kubwa.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh Yanga inalipa shilingi laki moja na nusu (150,000) kwa wakati mmoja ndani ya mwezi inalipa si chini ya Sh. 5mil kama inafanya mara mbili kwa siku yaani asubuhi na jioni au Viwanja vya gharama kama Gymkhana bei yake ni zaidi ya shilingi laki tatu (300,000) kwa wakati mmoja.

Yanga inatia nguvu katika ujenzi huo ili kuondokana na usumbufu pamoja na gharama za mazoezi.

Watani zao, Simba tayari wamekamilisha hatua ya upandaji wa nyasi kwa kiwanja cha kwanza cha nyasi asili huku ule wa bandia ukiwa kwenye mipango. Viwanja vyote viwili vya Simba vipo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

MRATIBU YANGA Hafidh Saleh alisema, kama uwanja huo utakamilika utawasaidia kwa vitu vingi.

“Tukiwa na uwanja wetu ina maana tutapunguza gharama. Hatutakuwa tunapoteza pesaa nyingi kwa ajili ya kukodi viwanja vya mazoezi. Kwani huwa tunalipa shilingi laki moja na nusu (150,000) ambazo ni nyingi kwa mara moja tu,” alisema Hafidh.

BILIONEA GSM KUFANYA YAKE

Mtu wa ndani wa GSM ameweka wazi kwa sasa mkataba wao ni kukarabati jengo la Yanga na pitch wanachangia ili zoezi hilo likamilike.

Ukarabati wa jengo hilo ni kulifanya kuwa katika hadhi ya hoteli kubwa ambazo timu hiyo imekuwa ikiweka kambi na itagharimu kati ya Sh.150 milioni hadi Sh. 200 milioni.

“Tutakalabati jengo liwe katika mandhari ya kisasa kabisa vyumba vyote (viko 30), viwe na AC, kuwe na swiming pool na vitu vyote ambavyo vitalifanya jengo hilo kuwa la kisasa kama hoteli kubwa.

“Lengo ni kwamba, timu itakapoweka kambi hapo kusiwe na tofauti na sehemu nyingine hii itapunguza gharama za hoteli, pia kutakuwa na duka kubwa la vifaa vya Yanga kama jezi, skafu na vyote.”

Alisema, mpango wao Yanga iwe kama Klabu ya Fenerbehce na hata ujenzi utakuwa hivyo na ukarabati huo unatarajiwa kuanza mwishoni mwaka huu.

“Kwenye uwanja GSM itachangia sehemu ya pesa kama msaada tu, lakini haiko kwenye makubaliano labda katika awamu nyingine,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alipoulizwa juu ya taarifa hizo alisema:

“Kuhusu marekebisho ya jengo, walikuja mafundi wa GSM wakafanya tathmini wakaondoka hawakutuambia gharama ni kiasi gani. Na sisi bado hatujafanya.”

MIUNDO MBINU

Dismas Ten alisema, mbali na kampuni hizo kufanya shughuli hizo Yanga ina Kamati ya Ujenzi na Miundombinu ambayo itafanya tathimini kwa upande wake.

Kamati ya Ujenzi na Miundombinu ipo chini ya Mwenyekiti, Bahati Mwaseba alipolizungumzia hilo alisema:

“Kamati bado haijaanza kazi bado, hivyo kwa sasa jukumu bado liko kwa Kaimu Katibu, Makamu Mwenyekiti na Mwenyekiti.”

Chanzo: mwananchi.co.tz