Dar es Salaam. Sakata la mshambuliaji nguli wa Simba, John Bocco kulimwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, limechukua sura mpya, baada ya beki wa Mwadui, Revocatus Mgunga kuanika sababu ya mzozo baina yao.
Bocco alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 81 na mwamuzi Alfred Vitalis wa Kilimanjaro kwa kumpiga ngumi ya kisogo beki huyo katika mchezo wa Ligi Kuu ambao Simba ilishinda mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mgunga alidai hana tatizo na Bocco na ameshangazwa na kitendo cha kupigwa ngumi wakati mchezo ukiendelea.
Mgunga alidai Bocco alikuwa akimtolea maneno makali muda wote na hakutaka kumjibu kwa kuwa ilikuwa ni sehemu mchezo akihofia kupewa kadi na mwamuzi.
“Inawezekana alichukia kwa sababu nilimdhibiti, lakini sina tatizo na Bocco (John). Nimesikitika kwa sababu aliyefanya kitendo hiki ni mchezaji mkubwa na kiongozi uwanjani.
“Ukiangalia kwa makini marudio ya mkanda wa video utaona sikuwa na kosa, nilikuwa natimiza wajibu wangu kama beki na sikumchezea rafu, mimi nahisi aliamua kunipiga kwa kuwa nilimbana,”alisema Mgunga.
Hata hivyo, beki huyo alikiri kumuumiza Bocco na kushindwa kuendelea na mchezo katika mechi ya msimu uliopita iliyochezwa kwenye uwanja huo na timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2.
Katika mchezo huo uliokuwa na ubabe mwingi baina ya wachezaji wa timu hizo, mshambuliaji huyo alifunga bao moja na jingine lilifungwa na Emmanuel Okwi kwa mkwaju wa penalti.
Bocco, alipotafutwa kuthibitisha madai ya mchezaji huyo, simu yake ya mkononi ilikuwa ikiita muda mrefu bila kupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.
Akizungumzia athari ya kukosekana Bocco katika mchezo huo, mratibu wa klabu hiyo Abbas Selemani, alisema wamejiandaa vyema na benchi la ufundi linatarajia kumpa nafasi mchezaji atakayeziba pengo la Bocco.
“Kwasasa siwezi kuzungumzia kadi nyekundu ilivyopatikana, lakini kwa kifupi Bocco hawezi kutuathiri katika mchezo wetu na Yanga kwa sababu Simba ina wachezaji wengi hodari ambao wana uwezo mzuri wa kucheza soka,” alisema Selemani.
Mratibu huyo alisema kuwa licha ya nahodha huyo kutokuwepo katika mchezo huo, Simba ina nafasi nzuri ya kushinda kwa kuwa wachezaji wameandaliwa vyema na benchi la ufundi chini ya kocha Patrick Aussems.
Kadi nyekundu itamuondoa Bocco katika mchezo unaofuata dhidi ya Yanga utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ingawa anaweza kuongezewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya 38 ya Ligi Kuu.
“Mchezaji atakayetolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kupiga/kupigana atasimama kushiriki michezo mitatu (3) inayofuata ya klabu yake na atalipa faini ya Shilingi 500,000 (laki tano),” inafafanua ibara ya tatu ya kanuni hiyo ya udhibiti kwa wachezaji.
Michezo mitatu ambayo mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya Azam atakosa ni dhidi ya Yanga, African Lyon na Stand United.