Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Bangi yamponza kiungo Yanga, afungiwa

25008 Pic+banka.png TanzaniaWeb

Thu, 1 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati ya Kupambana na Kuzuia Dawa Zisizoruhusiwa Michezoni Kanda ya Tano Afrika (RADO), imemfungia kiungo mpya wa Yanga Mohammed Issa ‘Banka’ kutojihusisha na soka kwa miezi 14.

Banka alisajiliwa na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, lakini hakuitumikia timu hiyo kwa kuwa muda mfupi alikwenda Kenya kushiriki mashindano ya Kombe la Chalenji akiwa na Zanzibar Heroes.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Clifford Ndimbo alisema, Banka alifanyiwa vipimo akiwa Machakos, Kenya ambapo alibainika anatumia bangi.

Ndimbo alisema kiungo huyo alifanyiwa vipimo Desemba 9, 2017 na majibu yalipotoka ilibainika anatumia dawa aina ya bangi ambayo hairuhusiwi katika mchezo wa soka.

Ofisa Habari huyo alisema Banka alikiri kwa kuandika barua kwamba alitumia dawa hizo na RADO ilitoa hukumu ya miezi 14 kutojihusisha na soka.

“Baada ya kukubali tuhuma Banka alipunguziwa adhabu kutoka kufungiwa maisha kutojihusisha na soka. RADO wanafanya kazi chini ya FIFA na CAF na wanaweza wakafanya maamuzi ya kuja nchini kufanya uchunguzi kwa wachezaji wa Ligi Kuu, Daraja la Kwanza na Pili jambo la msingi ni kwa wachezaji wetu kuacha kutumia dawa hizo.

“Tukio hili linafahamika FIFA na TFF tumejipanga kuzungumza na klabu zote kufanya vipimo kabla ya kusajili, matukio kama haya yakiwa mengi ligi yetu inaweza kupata matatizo,” alisema Ndimbo.

Alisema mchezaji huyo hatakiwi kufanya mazoezi katika viwanja vya wazi na endapo atatumikia vyema kifungo chake atapewa ruhusa ya kufanya mazoezi na timu kwa miezi miwili ya mwisho.

Pia Ndimbo alisema TFF inamtambua Banka ni mchezaji wa Mtibwa kwa kuwa Shirikisho hilo halikuwahi kutoa kibali cha kuitumikia Yanga baada ya kupata matatizo.

Winga wa Yanga, Emmanuel Martin alisema kukosekana kwa Banka kutapunguza morali ya timu hiyo ambayo ilimsajili kwa lengo la kuongeza nguvu msimu huu.

“Banka ana uwezo mkubwa wa soka na kukosekana kwake ni pigo, lakini tukio hili nadhani ni fundisho sina la kusema zaidi ya hapo,” alisema Martin.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alisema wanasubiri barua kutoka TFF na klabu itatoa taarifa rasmi kuhusu kufungiwa kwa mchezaji huyo.

“Kama klabu tumeguswa na tukio hili lakini tutakachofanya ni kuendelea kuwasiliana na Banka ili kutimiza vizuri adhabu yake na kupata ruhusa ya kufanya mazoezi na timu katika miezi miwili ya mwisho, lakini nina imani wachezaji wengine watachukulia tukio hili kama funzo kwao,” alisema Ten.

Daktari wa Taasisi ya Mifupa Hosipitali ya Taifa Muhimbili (MOI), Cathebert Mcharo alisema wachezaji wanaotumia bangi wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na presha.

Chanzo: mwananchi.co.tz