Klabu ya African Lyon imeandika barua nzito kwa washabiki wake, wadau wake wote na timu ya JKT Tanzania kufuatia matokeo waliyoyapata leo ya kufungwa kwa jumla ya mabao 5-1 kwenye mchezo wa ligi daraja la kwanza.
Kufuatia kipigo hicho African Lyon imetuma pongezi kwa JKT Tanzania kwa ushindi huo waliyoupata ambao sasa unawawezesha kurejea ligi kuu Tanzania Bara.
PONGEZI – JKT TANZANIA
Klabu ya African Lyon, inaomba msamahaa kwa washabiki wake na wadau wake wote kwa matokeo waliyoyapata leo ya kufungwa na timu ya mpira wa miguu ya JKT Tanzania. Kwenye mpira kuna kushinda, kutoa sare na kufungwa na wote tunakubali hilo lakini pale ambapo hatukubali ni timu inapocheza kwa kiwango ambacho hakionyeshi umuhimu wa majukumu waliyopewa. Kwa hilo ni budi kwetu sisi kuomba msamaha kwa wale wote wanaotutakia heri.Pamoja na pigo hili zito la kufungwa, African Lyon bado ingependa kuipongeza JKT Tanzania kwa mambo mawili. La kwanza ni kufanikiwa kwao kurudi kwenye Ligi kuu kwa kuweka rekodi nzuri sana msimu huu ulioonyesha wanastahili kabisa kupanda ligi.
Pongezi ya pili tunaitoa kama wanamichezo. Utayari, umakini, nidhamu ya timu nzima ya JKT Tanzania katika mechi ya leo ni fundisho kubwa sana kwa viongozi wetu na wachezaji wetu wote hapa Tanzania. Pamoja na kuwa wameshapanda daraja, mchezo waliouonyesha uwanjani ulikuwa ni wa ushindani wa hali ya juu na walikuwa na kila haki ya kupata ushindi. Mifano kama hii huwa tunaiona kwenye ligi za nje ambazo timu hucheza kwa nidhamu ya juu na uchu wa ushindi kuanzia mechi ya kwanza mpaka ya mwisho, bila kujalisha wako nafasi gani ya ligi.
Ni matumaini yetu sisi kama timu tumejifunza kwa kile tulichokiona leo na tunaahidi mashabiki wetu kwamba tutapambana mpaka dakika ya mwisho ya ligi na Mungu akijalia tutafanikiwa.
Charles Otieno,
Mkuu wa Benchi La UfundiAfrican Lyon FC
+1781 660 2017
[email protected]