Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems ataka haya aivushe Simba CAF

34188 Pic+simba Kocha wa Simba, Patrick Aussems

Tue, 1 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Patrick Aussems amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya droo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) huku timu yake ikipangwa Kundi D.

Droo hiyo ilifanyika mjini Cairo Ijumaa iliyopita na Simba ikipangwa na miamba ya Misri Al Ahly, JS Saoura (Algeria) na AS Vita ya DR Congo.

Akizungumza katika mahojiano mafupi na Mwananchi, Aussems alisema kundi lao la D ameliangalia akaona halimtishi na wala sio gumu ila ameomba mambo mawili ili aivushe timu.

Alisema mashabiki waendelee kuipa nguvu Simba kwamba wakipata sapoti ya mashabiki ninaamini mambo yatajipa.

“Mimi huwa sifanyi makosa, ninafahamu nini cha kufanya kama kufungwa itokee tunafungwa, lakini lazima nitafanya kitu.

“Nilifarijika kuona mashabiki mechi ya marudiano na Nkana, ile ndio inatakiwa kwa mashabiki kwani hata wachezaji wanapata nguvu ya kucheza. Sapoti ya mashabiki ni muhimu.

“Naamini hilo la mashabiki kuja litawezekana kwa sababu Watanzania wote kwa pamoja wanahitaji kuona timu ikisogea kutokana hakuna mwakilishi mwingine katika mashindano haya” alisema.

“Kingine nimewaambia wachezaji wangu, tuko kwenye hatua muhimu, siyo ngumu, muhimu hivyo ni lazima kujitoa kwa moyo mmoja katika michezo hiyo. Lazima kupambana kwa hali na mali kuhakikisha tunashinda.”

Aussems alisema kundi lao lipo wazi kwa wao kuvuka licha ya kwamba anatambua ugumu wa wapinzani wao katika mashindano hayo kutokana na uzoefu wa kushiriki mara kwa mara.

“Nina wachezaji ambao wana uwezo mkubwa wa kukabiliana na wapinzani hata wagumu, tunavyozidi kutumia nafasi kwa kufunga katika mechi za ligi ndio tunazidi kujiongezea kujiamini kuelekea katika mechi zetu za kimataifa,” alisema.

Kuhusu usajili alisema kwamba kutokana na dirisha la usajili nchini kufungwa, itamlazimu kutafuta mchezaji asiyekuwa na mkataba kama atahitaji kuongeza mchezaji.

“Sheria za Fifa zinatubana kufanya usajili kwa mchezaji ambaye ana mkataba , tunatakiwa tufanye usajili wa mchezaji ambaye yupo huru, tuna nafasi mbili mpaka tatu kufanya hivyo lakini muda tutajua baadaye,” alisema.

Mshambuliaji wa timu hiyo, Meddie Kagere aliiambia Mwananchi juzi kuwa wao kama wachezaji wana malebgo ya kufika mbali hivyo wanazichukulia timu hizo kwa uzito wake.

“Tunataka kushinda mechi zetu, kama mimi kazi yangu ni kufunga. Nataka kufunga ili kuifikisha mbali timu,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz