Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems: Mbabane imeinusuru Lipuli FC

28737 Pic+auseems TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kocha wa Simba, Patick Aussems amesema walishindwa kupata ushindi dhidi ya Lipuli kwa sababu akili za wachezaji wake zilikuwa zinafikiria mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland.

Simba itaikaribisha Mbabane, Jumatano ijayo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa raundi ya kwanza utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, kabla ya kurudiana kati ya Desemba 4 na 5 nchini Swaziland.

Alisema wachezaji wake walicheza mchezo wa juzi huku akili zao zikiuwaza mchezo dhidi ya Mbabane na hicho ndicho kilichoinusuru Lipuli kwani mkakati wao ni kupata ushindi wa kishindo Jumatano ili kujiweka katika nafasi nzuri katika mchezo wa marudiano.

Kocha huyo alisema mkakati wao kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni mkubwa sana na amewaeleza wachezaji wake umuhimu wa kupambana ili wafike mbali hivyo matarajio yake kufanya vizuri.

“Nimewaambia wachezaji kuwa tunapaswa kuwa makini na kujituma katika mechi zetu zote za Ligi ya Mabingwa Afrika tunataka kutumia michuano hii kuandika historia ndani ya Simba,” alisema Aussems.

Alisema moja ya faida watakazozipata ni kujitangazia soko lao nje, kwani michuano hiyo inafuatiliwa sana na mawakala na hata viongozi wa timu mbalimbali ndani na nje ya Afrika.

Bingwa wa mashindano hayo anapata Dola 2.5 milioni ambazo ni sawa na Sh 5.5 bilioni za Tanzania, bingwa wa msimu huu akiwa Esperance ya Tunisia iliyotwaa hizo fedha hizo baada ya kuishinda Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-3.

Aussems amewatoa hofu mashabiki wa Simba, akisema kuwa wataifunga Mbabane licha ya kuonyesha kiwango duni juzi dhidi ya Lipuli, akisema ameshafanyia kazi makosa yaliyofanywa na washambuliaji wake kushindwa kuzitumia nafasi walizozitengeneza.

Kiwango hicho kilianza kuwapa wasiwasi mashabiki wa Simba lakini Aussems amesema kuwa hawezi kuwashushia lawama washambuliaji wake John Bocco na Meddie Kagere kwa kukosa mabao juzi.

“Hata kabla ya mchezo huu sikuwa na uhakika wa kushinda kwa sababu nafahamu msimu uliopita Simba haikuishinda Lipuli katika mechi zote mbili na hii imekuwa moja ya timu ngumu dhidi ya Simba.

“Unajua wachezaji wangu juzi walikuwa wanafikiria zaidi mchezo wa Jumatano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, naomba mashabiki waiunge mkono tumekuwa tukifanya mazoezi ya ufungaji kwa wiki zaidi ya tatu sasa,” alisema.

Kocha huyo alisema mshambuliaji mahiri raia wa Uganda Emmanuel Okwi ambaye hakuwepo uwanjani juzi, atakuwepo Jumatano na atakuwa chachu ya ushindi.

Aussems aliwaomba wanachama na mashabiki kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu katika mchezo huo kwani uwepo wao ni chachu ya ushindi.



Chanzo: mwananchi.co.tz