Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aussems: Hata aje mwarabu, atapigwa tu

33795 Pic+simba Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likipanga ratiba ya makundi leo kwenye mji wa Cairo, Misri, kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema hiyo haiwatii presha kwani wako sawa na hata aje mwarabu, kipigi kiko palepale.

Simba iliingia kwenye hatua ya makundi baada ya kuibandua nje ya michuano, Nkana Red Devils ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3. Mchezo wa kwanza uliopigwa Kitwe, Simba ililala kwa mabao 2-1 kabla ya kuichana mabao 3-1 mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba ilianza safari yao ya kuwania ticketi ya kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye raundi ya awali kwa kucheza na Mbabane Swallows ya eSwatini.

Katika raundi hiyo, Simba ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mbao 8-1, walinza nyumbani kushinda 4-1 na wakamalizia ugenini kwa ushindi monono tena wa mabao 4-0.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara ya kwanza ni mwaka 2003 ambapo ilitinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 3-2 mbele ya Zamalek ya Misri na kuwavua ubingwa.

Tayari, timu 16 zimefuzu hatua hiyo na leo CAF inapanga makundi kwa ajili ya mwendelezo wa mechi hizo. Simba inawakilishwa na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’.

Shirikisho hilo limepanga vyungu vinne na kila chungu kina timu nne na kila chungu kitatoa timu moja kwenye kundi moja.

Vyungu hivyo vimepangwa kulingana na viwango vya ushiriki wa klabu michuano ya CAF kwa miaka mitano iliyopita.

Chungu namba moja kina klabu za TP Mazembe (DR Congo) yenye pointi 66, Al Ahly (Misri, pointi 62), Wydad Casablanca (Morocco, pointi 51) na Esperance de Tunis ya Tunisia yenye pointi 45.

Chungu namba mbili kinaundwa na klabu za Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) yenye pointi 40, AS Vita Club (DR Congo, pointi 29), Horoya (Guinea, pointi 19) na Club African ya Tunisia yenye pointi 12.

Chungu namba tatu ziko ASEC Mimosas (Ivory Coast, pointi 8.5), Orlando Pirates (Afrika Kusini, pointi nane), FC Constantine (Algeria) na FC Platinum (Zimbabwe) zenyewe hazina pointi.

Simba iko chungu namba nne pamoja na Lobi Stars (Nigeria), Ismaily (Misri) na JS Saoura ya Algeria na zote hazina pointi.

Kila chungu kitatoa timu moja kwa kila kundi, timu ambazo zipo chungu kimoja haziwezi kupangwa kundi moja hivyo Simba haiwezi kukutana na Lobi Stars, Ismaily wala JS Saoura.

Mechi za makundi zitaanza Januari hadi Machi na kutakuwa na makundi manne yenye timu nne na kila timu itacheza mechi sita ikiwa mechi tatu za nyumbani na mechi tatu za ugenini.

Kauli ya kocha Simba

Akizungumza na gazeti hili, Aussems alisema kwamba lengo kubwa na wachezaji wake lilikuwa ni kufanikiwa kuingia katika hatua hiyo ya makundi kwa hiyo hawezi kuwa na woga wowote ule.

“Lengo letu la kwanza tumeshalifanikisha, ninadhani tumepiga hatua, tulijua kabisa kwamba tukifika hapa kuna timu tunakutana nazo kwa hiyo kikubwa ni kujipanga tu,” alisema.

Aussems alifunguka zaidi na kusema kwamba lengo lake ni kuhakikisha klabu ya Simba inakuwa miongoni mwa klabu kubwa Afrika, huku akisisitiza kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.

“Tumefuzu tunatakiwa kuangalia mbele zaidi, Simba naweza kusema bado inaendelea kukuwa na lengo langu ni kuiona Simba ikiwa miongoni mwa klabu tano kubwa Afrika huko mbeleni,” alisema



Chanzo: mwananchi.co.tz