Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Arusha United yatangaza kujitoa Ligi Daraja la Kwanza, TFF yawajibu

47904 ARUSHA+PIC

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

ARUSHA. HATIMAYE timu ya Arusha United inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara imetangaza kujitoa kwenye mashindano hayo kwa kile walichodai kufanyiwa matukio yasiyo ya kimichezo wakieleza kuwa Bodi ya Ligi ya TFF ikishindwa kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo.

Akizungumza na gazeti hili Afisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema kuwa bado hawajapata barua rasmi kutoka Arusha United za kujitoa kwenye mashindano hayo ya FDL.

"Barua rasmi bado sijaiona na kama ingekuwepo basi Bodi ya Ligi ya TFF ingenipa taarifa ya cha kusema. Hivyo tunasubiri barua na hata barua isipokuja basi tutasubiri wasipotokea uwanjani mchezo wao unaofuata dhidi ya Pamba ndio hatua zitachukuliwa," alisema Ndimbo.

Ndimbo aliongeza kuwa endapo timu hiyo wakijitoa kwa barua rasmi au kutokwenda kucheza Mwanza basi watakuwa wameshushwa madaraja mawili (hadi ligi ya mkoa) na kufungiwa miaka miwili na adhabu nyingine bodi ya ligi ya TFF itakayoona inafaa ikiwemo kupigwa faini.

Akitangaza uamuzi huo mkurugenzi wa Arusha United, Otte Ndaweka alisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kufanyiwa vitendo wanavyodai ni vya kihuni katika viwanja vya ugenini hasa michezo dhidi ya Rhino rangers huko Tabora walioingiza wahuni zaidi ya 40 uwanjani wakiwa na silaha mbalimbali za jadi kama fimbo na nondo na kuwajeruhi baadhi ya wachezaji wao sambamba na viongozi wa timu.

Alisema mchezo mwingine ni dhidi ya Transit Camp ambapo walianza kufanyiwa vurugu tangu wanaingia tu na basi katika uwanja wa Azam Complex ambapo baadhi ya mashabiki wa timu hiyo waliingia uwanjani na chupa zenye mikojo wakitaka kuwamwagia wachezaji wao, lakini baadae walipuliza dawa vyumbani hali iliyowabidi kukaa nje vipindi vyote vya mapumziko huku wachezaji wao wakipigwa lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na viongozi wa TFF ingawa walikuwepo uwanjani.

"Mchezo mwingine tuliyofanyiwa vurugu ni dhidi ya Polisi Tanzania kule Moshi ambapo mbali na kutoa tahadhari kwa TFF dhidi ya viashiria vya vurugu na kujaza askari uwanjani wanaosababisha hali ya taharuki kwa mashabiki wa michezo lakini hakuna hatua iliyochukuliwa zaidi ya vitendo hivyo kujirudia na kwetu ambapo walishindwa hata kuheshim kibali cha shirikisho la kuruhusu michezo kurekodiwa bali walimvuta mwandishi wetu kutoka juu ya gari na kumjeruhi vibaya licha ya mkuu sa wilaya ya Arumeru Jerry Murro kuwatuliza bila mafanikio."

Ndaweka alisema kuwa kufuatia matukio hayo yote kufanyika imehatarisha usalama wa wachezaji na viongozi wote kwa ujumla na kwa sababu bodi ya TFF imeshindwa kuchukua hatua, wameamua kujitoa kwenye mashindano hayo kwa lengo la kusisitiza Shirikisho kuelekeza macho yao kwenye ligi hiyo.

"Tumekaa bodi nzima ya udhamini na kuona mambo yanayoendelea huko kwenye mashindano ni uhuni mtupu na TFF hawana historia ya kuchukua hatua juu ya matukio hayo, hivyo ili kutokuonekana na sisi ni wahuni tumeona bora kujitoa kulinda heshima yetu lakini pia kuishtua shirikisho kuongeza umakini katika ligi hii na jicho la kipekee lielekezwe kwa timu zilizobakia."

 

 



Chanzo: mwananchi.co.tz