Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Angola ina kiu

44790 Angola+pic Angola ina kiu

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kati ya timu zinazojipanga kwelikweli kwa michuano ya Vijana ya U-17 itakayofanyika nchini ni Angola.

Pamoja na timu hiyo kupeleka vijana wake kwenye michuano ya UEFA Assit inayoanza leo Uturuki, timu hiyo ilikuwa nchini Ureno kwa maandalizi ya michuano hiyo na ile ya hapa nchini.

Angola imekuwa nchini Ureno, imepangwa kundi moja na Serengeti Boys kwenye Fainali hizo za Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye miaka 17.

Fainali hizo zitafanyika hapa nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28 na zitashirikisha timu nane huku Kundi A likiwa na timu za Angola, Uganda Nigeria na wenyeji Serengeti Boys.

Kundi B lina timu za Cameroon, Senegal, Morocco na Guinea.

Angola na Serengeti Boys ni timu zinazofahamiana vizuri kwa kuwa zimeshacheza mara kadhaa katika siku za karibuni.

Pamoja na kupangwa kundi moja kunaifanya siku watakayokutana kuwa bonge moja la mechi kutokana na ubora wa timu zote mbili.

Timu hizo ndani ya miaka miwili zimekutana mara tatu ukiwemo mchezo wa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017, Angola iliposhinda mabao 2-1 nchini Gabon.

Pia zilikutana mwaka jana kwenye mashindano ya vijana ya COSAFA (Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika) na katika hatua ya makundi Angola iliichapa Serengeti Boys mabao 2-0 lakini vijana wa Tanzania wakalipiza kisasi katika mchezo wa fainali kwa kushinda penati 6-5 baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90.

Hawa ni hatari

Angola inabebwa sana na wachezaji Abdoul Maliki Barri, Zito Luvumbo na Osvaldo Pedro Capemba . Inaongozwa na nahodha Jose Nguna Cabingano ambaye ni beki lakini pia ni mzuri wa kufunga mabao ya vichwa.

Mshambuliaji Zito ameonekana kuwa na mchango zaidi ndani ya timu hiyo kwani si mahiri katika kufunga tu lakini pia ni mzuri kwa pasi za mwisho na anatisha kwa kufunga mabao ya faulo.

Wachezaji hao pia waliongoza kwa kufunga katika mashindano ya Coasafa, Barri akiwa amefunga mabao manne na Capemba na Luvumba wakifunga matatu kila mmoja.

Hata hivyo, Barri na Capemba hizi ndio zitakuwa fainali zao za mwisho kuichezea timu hiyo chini ya miaka 17 kwani mwakani watakuwa wamefikisha miaka 18.

MAFANIKIO

Mafanikio ambayo timu hiyo imepata ni kushiriki Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 mwaka 1997, 1999 na 2017 lakini iliishia hatua ya makundi .

KUFUZU

Angola inayofahamika kwa jina la utani la OS Palanquinhas ilipata nafasi ya kushiriki fainali hizi baada ya kutwaa ubingwa wa nchi za Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (Cosafa).

Timu hiyo ilianza kuifunga Malawi bao 1-0 kisha ikailaza Swaziland mabao 4-0, mabao yakifungwa na Zito aliyefunga mawili, Domingos Andrade na nahodha Jose Cabingano.

Timu hiyo ilimaliza hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Zimbabwe.

Kwenye nusu fainali ilichapa Namibia mabao 7-0 yaliyofungwa na Osvaldo Capemba aliyefunga hat-trick, Gaspar Morais alifunga mawili wakati mengine yalifungwa na Zito na Barri.

Timu hiyo ilibeba ubingwa wa Cosafa kwa kuifunga Afrika Kusini kwenye fainali kwa bao 1-0.

KIKOSI

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Angola kinanolewa na kocha Love Cabungula na kinaundwa na makipa Edmilson Cambila na Geovani de Carvalho wakati mabeki ni Cristiano Rocha, Domingos Andrade, Telson Tome, Adriano Ndonga, Afonso Binga, Rivaldo Cambuta na Jose Cabingano.

Viungo ni ni Manuel Londaka na Pedro Banga wakati washambuliaji ni Osvaldo Capemba, David Nzanza, Zito Luvumbo, Abdoul Barri, Francisco Junior na Gaspar Morais.



Chanzo: mwananchi.co.tz