Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amunike awaibua wadau Taifa Stars

14645 AMUNIKE+PIC TanzaniaWeb

Thu, 30 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Giza nene limetanda kwenye kambi ya timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ siku tisa kabla ya mchezo muhimu wa ugenini wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika dhidi ya Uganda, baada ya nyota sita wa Simba kutimuliwa katika kikosi hicho kwa utovu wa nidhamu.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike, amewaondoa katika kikosi hicho wachezaji Shiza Kichuya, Erasto Nyoni, John Bocco, Jonas Mkude, Hassani Dilunga, Shomari Kapombe na Feisal Salum wa Yanga.

Hata hivyo, wakati uamuzi huo ukitolewa jana saa sita mchana na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wilfred Kidao, Kapombe alidai yuko kambini.

Kidao alisema wachezaji hao wameondolewa katika kikosi hicho siku mbili tangu kambi ya Taifa Stars ilipoanza baada ya kushindwa kuripoti kambini ndani ya muda uliopangwa.

Kipa Aishi Manula, amekwepa adhabu hiyo baada ya kuwasili kambini katika muda uliopangwa ambao ulikuwa jana saa 12:00 asubuhi. Taifa Stars na Uganda ‘The Cranes’ zinatarajiwa kumenyena Septemba 8 mjini Kampala.

Amunike ameita sura mpya kujaza nafasi za wachezaji hao ambazo ni Salum Kimenya (Prisons), Paul Ngalema, Ally Abdukadir (Lipuli), David Mwantika, Frank Domayo (Azam), Kelvin Sabato na Salum Kihimbwa kutoka Mtibwa Sugar.

Uamuzi wa Amunike, umepongezwa na baadhi ya wadau wa soka ambao walisema kocha yuko sahihi kwa kuwa anataka kujenga timu yenye nidhamu.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu, alisema Amunike yuko sahihi kuchukua uamuzi huo ili kujenga nidhamu kwa wachezaji.

Kipingu alisema ingawa wachezaji wa Simba hawana rekodi ya utovu wa nidhamu, lakini walipaswa kutoa taarifa kwa wahusika kuwa wangechelewa kuripoti kambini.

“Kama Aishi Manula aliwahi wengine walikuwa wapi? Hiyo ni nidhamu mbovu maana wote watakuwa waliambiwa. Mwanzoni kwa fikra zangu niliona kama hawakutendewa haki kwa kuwa TFF ilipaswa kuwasiliana na klabu kuwaombea ruhusa.

“Lakini baadaye nilibaini Manula alikuwepo kambini bila shaka wengine walichelewa kwa utashi wao,” alisema Kipingu.

Kipa nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mohammed Mwameja alisema kocha yuko sahihi kuchukua uamuzi huo kwa kuwa nidhamu ndio njia pekee ya mafanikio katika soka.

“Sisi zamani kama kocha akiwaambia mazoezi saa mbili, muda huo wote mnakuwepo asiyekuwepo lazima awe na sababu za msingi, nidhamu ni kitu kikubwa sana kwenye timu na kocha yuko sahihi kuwaondoa waliochelewa, labda wawe na sababu za msingi,” alisema Mwameja.

Naye kinara wa mabao wa zamani ya Yanga na Taifa Stars, Peter Tino alisema uamuzi wa kocha huyo ni mzuri na ameonyesha msimamo mapema katika kusimamia nidhamu.

“Mnapokuwa kwenye timu halafu wengine wanajiamulia watakavyo hiyo siyo timu, alichofanya kocha ni sahihi kabisa na utaratibu huo uwe endelevu,” alisema Tino.

Kocha na mchambuzi wa soka Kennedy Mwaisabula, alisema Amunike amefanya uamuzi stahiki kwa kuwa wachezaji wa Tanzania wamekuwa na utovu wa nidhamu.

“Mimi nikiwa kama mwalimu sipendi mchezaji asiyekuwa na nidhamu, hata wewe ni mwajiriwa unapoambiwa ufike muda fulani kazini lazima ufike katika muda huo, mbona kipindi cha (Marcio) Maximo walivyokuwa wakipewa taarifa walikuwa wanafika siku moja kabla,” alisema Mwaisabula aliyewahi kuinoa Yanga.

Awali, Kidau alisema Amunike alichukua uamuzi huo kwa kutoridhishwa na kitendo cha wachezaji hao kushindwa kuripoti kambini licha ya kupewa taarifa mapema.

“Walitakiwa kuingia kambini jana, lakini mchezaji aliyefika alikuwa Aishi Manula na wengine walishindwa kuripoti, nilizungumza na baadhi ya wachezaji wa Simba na kuwaeleza hali halisi.

“Lakini kinachoonekana hawakupata taarifa kwa wakati licha ya sisi kupeleka barua mapema. Uamuzi wa mwalimu tunaunga mkono kwa sababu Taifa Stars inahitaji maandalizi na hakuna mtu ambaye yuko juu ya timu,” alisema Kidao.

Katibu Mkuu huyo alisema TFF imewaita Kaimu Katibu Mkuu wa Simba, Hamisi Kisiwa na Meneja Robert Richard kwenda kutoa maelezo kwa Kamati ya Maadili ya shirikisho hilo kuhusu mkanganyiko huo.

“Tumewaita ili kupata majibu kwa sababu wao ni miongoni mwa watu waliopokea barua ya wachezaji kuitwa. Niliongea na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘TryAgain’ na alimuagiza ahakikishe wachezaji wanafika kambini leo (jana),” alisema Kidao.

Kidao alisema sababu ya kuwaita kambini mapema wachezaji wa Taifa Stars wanaocheza ligi ya ndani ni kumpa muda wa kutosha Amunike kuwaandaa vyema kabla ya kuivaa Uganda.

“Kocha alifuatilia mikanda ya michezo iliyopita na alibaini baadhi ya makosa, hivyo alihitaji kukaa na wachezaji kwa muda ili afute makosa hayo kwa kuanza na wachezaji waliopo nyumbani,” alisema Kidao.

Meneja wa Simba aliliambia gazeti hili amepokea wito wa kuitwa na TFF na atakwenda mbele ya kamati ya maadili kutoa maelezo.

“Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa nitakwenda kuzungumza katika kamati kwa sababu ndiko nimeitwa kwenda kutoa maelezo, nikimaliza nitakuwa na muda mzuri wa kuzungumza,”alisema Richard kwa ufupi.

“Kama mchezaji ameteuliwa, anatakiwa aruhusiwe kujiunga na chama cha nchi yake. Muda wa kuruhusiwa unatakiwa uwe saa 48 kabla ya mchezo,” kinasema kifungu (C) cha muongozo wa kanuni ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).

Chanzo: mwananchi.co.tz