Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amunike: Tanzania tutakwenda Afcon

47829 AMUNIKE+PIC

Thu, 21 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike amewataka Watanzania kuamini kuwa timu hiyo itaibuka na ushindi dhidi ya Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Jumapili na kukata tiketi ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika Misri mwezi Juni.

Taifa Stars inalazimika kushinda dhidi ya Uganda huku ikiomba dua kwa Cape Verde kuibuka na ushindi ama kutoka sare na Lesotho ili kuungana na Uganda kufuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Amunike alisema Taifa Stars ina uwezo wa kuifunga Uganda kwa kuwa ana kikosi imara, inafanya maandalizi ya kutosha na inabebwa na faida ya kucheza nyumbani.

“Tunapaswa kuamini ndoto zetu ziko hai na zinaweza kutimia. Maandalizi ambayo tunaendelea kufanya yananipa matumaini timu inaweza kufanya kile ambacho tunahitaji na nimewaambia wachezaji wangu wasahau kile kilichotokea nyuma na kurekebisha makosa tuliyofanya yasijirudie katika mchezo huu.

“Naifahamu Uganda ni timu ngumu ina wachezaji wazuri lakini hatuwaogopi. Hautakuwa mchezo rahisi kwetu kutakuwa na nyakati tutakuwa juu na chini ingawa kwetu tutakuwa na faida ya kucheza nyumbani,” alisema Amunike.

Amunike alisema kutokana na ubora wa wapinzani wao, Taifa Stars haitacheza kwa kujilipua japo ina ulazima wa kuibuka na ushindi katika mchezo huo.

“Tunatakiwa kuwa na uwiano mzuri wa kujilinda na kushambulia ndio maana hata wachezaji ambao nimewaita nimeangalia wale ambao wataweza kufanya kitu pindi tunapokuwa na mpira, lakini tutakapopokonywa wahusike katika kuusaka,” alisema Amunike.

Alisema uwepo wa nyota 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiongozwa na nahodha Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji umeongeza morali ya ushindi.

“Kwa wachezaji morali ipo juu na ukizingatia nyota wote wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wamefika kwa wakati na kuwa na mwitikio chanya naamini watakuwa chachu kwa wengine kikosini,” alisema Amunike.

Nyota wengine wanaocheza soka la kulipwa ni Rashid Mandawa (BDF XI), Hassan Kessy (Nkana), Saimon Msuva (Difaa el Jadida), Thomas Ulimwengu (JS Saoura), Farid Musa (CD Tenerife), Shabani Chilunda (CD Izarra), Himid Mao (Petrojet), Shiza Kichuya (ENPPI) na Yahya Zayd (Ismaily)

Taifa Stars inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi hilo, iwapo itaibuka na ushindi dhidi ya Uganda itafikisha pointi nane ambazo zinaweza kuivusha ikiwa Lesotho yenye pointi tano itapoteza au kutoka sare na Cape Verde yenye pointi nne.

Hata hivyo, ndoto ya Taifa Stars kufuzu Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 zitafutika rasmi hata kama itaifunga Uganda iwapo Lesotho itaibuka na ushindi ugenini kwa kuwa zitakuwa na idadi sawa ya pointi.

Taifa Stars itaondoshwa kwa sheria ya kutokuwa na matokeo mazuri mbele ya Lesotho pindi timu hizo zilipokutana katika mechi mbili baina yao.



Chanzo: mwananchi.co.tz