Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Amunike: Kumradhi Watanzania, ila mwiko kukata tamaa

27942 Pic+stars TanzaniaWeb

Tue, 20 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' Emmanuel Amunike amewaomba radhi Watanzania kwa matokeo mabaya dhidi ya Lesotho, huku akiwataka kuendelea kuiunga mkono timu hiyo ili mwisho wafurahi pamoja wakiwa Cameroon.

Taifa Stars ilifungwa ugenini bao 1-0 na Lesotho katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zitakazofanyika mwakani nchini Cameroon.

Kutokana na matokeo hao Taifa Stars imejiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwani itabidi iifunge Uganda Machi mwakani na Cape Verde aifunge Lesotho ili iweze kufuzu.

Taifa Stars iko nafasi ya pili kwenye kundi L ikiwa na pointi tano sawa na Lesotho, lakini zikitofautiana idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa. Uganda ndio inaongoza kundi hilo ikiwa na pointi 13 na tayari imeshafuzu Afcon.

Taifa Stars imefunga mabao matatu sawa na Lesotho lakini Stars imeruhusu mabao matano huku Lesotho ikiruhusu mabao saba.

Amunike alisema anaheshimu maoni ya kila mtu, lakini mpira wa miguu wakati mwingine huwezi kutabiri kitakachotokea.

"Nawaomba radhi kwa dhati Watanzania wote sababu walikuwa na matumaini makubwa na timu yao, lakini naomba niwakumbushe kwamba bado tuko kwenye mbio, tupo nafasi ya pili licha ya kupoteza hivyo bado tuna nafasi ya kufuzu Afcon.

"Tunaweza kuwa na hasira kama taifa, tunaweza kuwa na hasira kwa mtu mmoja mmoja pia tunaweza kuwa na hasira wote, lakini tutambue jambo la muhimu ni kuwa tuna nafasi moja kubwa kucheza dhidi ya Uganda mwakani na kushinda.

"Tuna nafasi ya kufuzu, kwa hiyo maoni ya kila mtu yaheshimike, hasira ya kila mtu iheshimike.

Nimecheza mpira najua watu wanavyojisikia lakini nawaomba kuwa wajue safari haijaisha pia tunawahitaji zaidi waendelee kuiunga mkono timu. Tunawahitaji sana ili mwisho wa safari hii wote tufurahi kuwa tupo Cameroon,"alisema Amunike.

 

Naye nahodha wa Taifa Stars, Erasto Nyoni amewaomba Watanzania kuwavumilia kwani matokeo mabaya waliyopata hayakuwa matarajio yao.

"Watanzania watuvumilie kwa kipindi hiki kwani matokeo haya yametuumiza kwa sababu hatukuyatarajia kwani malengo yetu yalikuwa kupata ushindi.

 "Tumerudi nyumbani ili kujipanga vizuri na mechi inayofuata tufanye vizuri. Watanzania wasitutupe na waamini kuwa tunaweza kupambana mpaka dakika ya mwisho ili tuweze kufuzu," alisema Nyoni.

Bado kuna nafasi 11 zimebaki kwa timu kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2019, zote zitaamuliwa na mechi za mwisho.

Madagascar, Tunisia, Misri na Senegal zilikuwa za kwanza kufuzu pamoja na wenyeji Cameroon timu nyingine nane zilipata tiketi wiki hii ni Morocco, Nigeria, Uganda, Mali, Guinea, Algeria, Ivory Coast na Mauritania.

Mauritania na Madagascar zimefuzu kwa mara ya kwanza kwa Afcon, wakati Nigeria ‘Super Eagles’ imerejea kwa mara ya kwanza tangu ilipotwaa ubingwa huo miaka mitano iliyopita Afrika Kusini.



Chanzo: mwananchi.co.tz