Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ambani aing'ata Yanga sikio kuwika

Ambanibony Boniface Ambani

Wed, 15 Jul 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

STRAIKA hatari wa zamani wa Yanga, Boniface Ambani ameonyesha kusikitishwa na timu yake hiyo ya zamani kufungwa mabao 4-1 dhidi ya watani zao wa jadi Simba na kuwataka viongozi wa klabu hiyo kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wanaoendana na hadhi ya klabu.

Akizungumza kutoka nchini Kenya jana, Ambani ambaye ni mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2008/09, akipachika jumla ya mabao 18 akiwa na Yanga, alisema kwa sasa anavyoitazama Yanga ina wachezaji wengi ambao hawana hadhi ya kuichezea klabu kubwa kama hiyo.

"Niliwaona wakicheza na Kariobangi Sharks mwaka jana kabla ya msimu huu haujaanza, nilishangaa na nikatoa maoni yangu kwenye mtandao wangu wa kijamii kuhusu mapungufu makubwa ya kikosi, lakini nilikashifiwa sana na baadhi ya watu," alisema Ambani ambaye ni raia wa Kenya.

Mchezaji huyo ambaye amejinasibu pia kuwa pamoja na shughuli zake zingine amebaki kuwa shabiki mkubwa wa Yanga, alisema amesikitishwa mno timu hiyo kufungwa na Simba na kusema kuwa inafaa sasa kukifanyia mabadiliko makubwa kikosi hicho.

"Ikiwezekana wasisajili kabisa wachezaji 30, wasajili 25 tu, halafu ile gharama ya kusajili wachezaji watano, waiongezee kwa wachezaji hawa hawa 25 ili wapate nyota wenye gharama kubwa na wa viwango vya juu," alisema.

Ambani pia alikumbushia juu ya yeye kutoa tahadhari ya kutomsajili straika kutoka Ivory Coast, Gnamien Yikpe kutoka Gor Mahia ya Kenya, lakini alidharauliwa.

"Kila kitu nilichokuwa nikitolea ushauri au tahadhari, basi nilikuwa naandikiwa maneno makali na kukashifiwa kwenye mtandao wangu wa kijamii, maana hata hili suala la Yikpe, mimi nilitoa tahadhari ya kutomsajili, kwa sababu mimi namfahamu vizuri alikuwa hapa nchini Kenya akiichezea Gor Mahia, wananidharau na leo hii nadhani wameyaona," alisema straika huyo wa zamani wa klabu hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live