Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajibu augua ghafla Yanga

56436 AJIB+PIC

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

  Dar es Salaam. Nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajibu ameugua ghafla muda mfupi kabla timu hiyo kupanda ndege kwenda Mwanza kujiandaa na mchezo wake wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United.

Yanga itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Karume, mkoani Mara kuwania pointi tatu katika mchezo utakaofanyika kesho.

Akizungumza kwa simu jana akitokea Musoma, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema Ajibu aliugua ghafla homa akiwa anajiandaa kwa safari hiyo.

“Ibrahim Ajibu amepata homa muda mfupi kabla ya kuondoka, hivyo hatukuweza kusafiri naye pamoja na Gadiel Michael ambaye hajapona vizuri, lakini wachezaji wengine wako katika kiwango kizuri kwa mchezo huo,” alisema Zahera.

Kocha huyo raia wa DR Congo alisema licha ya kutokuwepo Ajibu, wamejiandaa kucheza kwa ushindani na lengo ni kupata ushindi katika mchezo huo.

Zahera alisema hawezi kukata tamaa kwa kuwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara uko wazi na timu yoyote ina nafasi ya kutwaa.

“Sitaki kujua habari za timu nyingine kila mmoja anapambana kivyake, lakini naamini ubingwa bado huko wazi.

“Matokeo ya nani anafanya nini hayatuhusu, ninachotaka tumalize mechi zetu zote zilizobaki kwa ushindi, bado tunaamini ubingwa upo wazi,” alisisitiza Zahera.

Yanga imebakiwa na mechi nne dhidi ya Biashara United (Musoma), Ruvu Shooting, Mbeya City na Azam (Dar es Salaam) ambazo kama itashinda zote itafikisha pointi 90.

Simba ambao ni watani wao wa jadi, kama watashinda mechi zote ikiwemo ya jana dhidi ya Coastal United itafikisha pointi 102 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine kwenye mashindano hayo.

Ukiondoa mechi ya jana, Simba imebakiwa na mechi dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC, Ndanda, Biashara United (Dar es Salaam), Singida United (Singida) na Mtibwa Sugar (Morogoro).

Yanga ambayo ilisafiri kwa njia ya barabara ikitokea Mwanza kwenda Musoma, ilipata mapokezi kabambe baada ya mashabiki wilayani humo kusindikiza gari la timu hiyo huku jina Zahera likitajwa.

Kocha huyo alisema mapokezi hayo ni dalili njema kwa Yanga na matumaini yake ni kupata pointi tatu.



Chanzo: mwananchi.co.tz