Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ajibu, Makambo ukinuna mchawi

23268 Ajib+pic TanzaniaWeb

Mon, 22 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Ukisikia Ibrahim Ajibu au Haritier Makambo ujue wamefunga au mmoja katoa pande likatengeneza bao, lazima utacheka kwa shangwe au kutabasamu.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa jana Uwanja wa Taifa wakati Yanga ilipoibanjua Alliance ya Mwanza mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Ushindi huo umeifanya Yanga kupanda hadi nafasi ya pili katika msimamo, ikifikisha pointi 19 mbili nyuma ya vinara Azam FC, ikiishusha hadi nafasi ya tatu Mtibwa Sugar yenye pointi 17, lakini Yanga ikiwa na mechi mbili za kiporo.

Katika mchezo wa jana, Yanga ilianza kujipatia bao la kuongoza katika dakika ya 17 lililofungwa na Makambo alipoitendea haki pasi murua ya Ibrahim Ajibu.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 25 aliyeunganisha pia pasi nzuri ya Ajibu ambaye aliendelea kung’ara msimu huu kwa kupiga pasi nyingi za mabao na Yanga kwenda mapumziko ikiongoza kwa mabao 2-0.

Kipindi cha pili Yanga ilikianza kwa kasi ile ile lakini iliishia kucheza mpira wa kufurahisha mashabiki wao jukwaani badala ya kutafuta zaidi mabao.

Bao la tatu la timu hiyo lilifungwa na Ibrahim Ajibu dakika ya 86 kwa shuti kali akiwa nje ya 18 baada ya kupata pasi ya Deus Kaseke aliyeingia katika dakika ya 61, kuchukua nafasi ya Ngassa.

Matokeo ya mechi nyingine za ligi hiyo zilizochezwa jana yalitawaliwa na sare ya bila mabao, Biashara United ya Mara ilibanwa na KMC ya Kinondoni, Tanzania Prisons ikiwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya ikashindwa kuitambia Singida United baada ya suluhu.

Mkoani Tanga, wenyeji Coastal Union nayo ilishindwa kutamba licha ya kuwa kwenye Uwanja wake wa nyumbani wa Mkwakani, baada ya kulazimishwa suluhu na maafande wa JKT Tanzania.

Chanzo: mwananchi.co.tz