Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Aiyee, bunduki ya Mwadui tishio kwa Kagere, Makambo

44799 Mwadui+pic Aiyee, bunduki ya Mwadui tishio kwa Kagere, Makambo

Tue, 5 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukiuliza mashabiki wa soka nchini mshambuliaji gani hatari katika Ligi Kuu Tanzania Bara, jibu rahisi watakwambia Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na Heritier Makambo.

Kagere, Okwi (Simba) na Makambo anayecheza Yanga wote ni wachezaji wa kigeni na majina yao yanatawala midomoni mwa mashabiki kutokana na ubora wao wa kufunga mabao.

Pamoja na ubora wa nyota hao, lakini lipo jina geni masikioni mwa mashabiki wa soka ambalo ni Salim Aiyee anayecheza Mwadui ya Shinyanga.

Licha ya kutofahamika kwa wadau wa soka, lakini Aiyee ndiye mtu tishio zaidi kwa nyota hao watatu wanaowania kiatu cha dhahabu msimu huu.

Aiyee kwasasa ndiye habari ya mjini, kwani uwezo wake wa kufunga mabao umewaweka kando Kagere, Okwi na Makambo na haitashangaza akitwaa tuzo ya mfungaji bora msimu huu.

Sifa moja kubwa ya mshambuliaji ni kufunga mabao na Aiyee amefaulu kigezo hicho kwani mpaka sasa anaongoza kwa idadi ya mabao akiwa amepachika wavuni 14.

Ubora wake wa kufunga mabao katika mashindano hayo, tayari umeanza kumuweka mawindoni kwa miamba ya soka Simba na Yanga. Aiyee anayecheza msimu wa tano katika Ligi Kuu, anaongoza akifuatiwa na Makambo mabao 12 sawa na Kagere, Said Dilunga wa Ruvu Shooting aliyefunga 10.

Simba na Yanga

Ndoto ya idadi kubwa ya wachezaji ni kucheza Simba au Yanga, lakini kwa Aiyee imekuwa tofauti, anasema hana mpango huo kwa kuwa ana mkakati kabambe wa kucheza soka Ulaya.

Anasema ingawa Simba na Yanga ni klabu kubwa lakini akili yake ni kucheza Azam FC akiamini ni sehemu salama kwa masilahi na kupata nafasi ya kucheza.

Taifa Stars

Aiyee anasema juhudi zote anazofanya uwanjani kwasababu ya Taifa lake, anapenda siku moja kuvaa ‘uzi’ wa timu ya Taifa, Taifa Stars.

Anasema anataka kutoa mchango wake kwa Taifa kupitia soka na ametoa wito kwa benchi la ufundi kumtupia jicho katika mechi ijayo ambayo Taifa Stars itacheza na Uganda kusaka tiketi ya kufuzu Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

“Natamani kucheza timu ya Taifa ninaamini siku nikipata nafasi nitafanya vizuri kwasababu hii ni nchi yangu, iweje nifunge katika Ligi Kuu nishindwe kimataifa,” anasema Aiyee.

Afrika Kusini

Pamoja na kuonyesha uwezo katika Ligi Kuu, lakini mkakati wa Aiyee ni kucheza soka Afrika Kusini kwa kuwa anavutiwa na ubora wake.

Anasema malengo ya kucheza soka Afrika Kusini yatatimia tu endapo ataongeza juhudi na maarifa katika ligi ya ndani ambao ndio mkakati wake.

Anasema msingi wake wa kucheza soka nje upo mikononi mwa Mwadui kwa kuwa anaishi katika mazingra mazuri na klabu hiyo inamuamini.

Kiatu cha dhahabu

Licha ya ubora wa Kagere, Okwi na Makambo lakini Aiyee hana hofu katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora katika Ligi Kuu msimu huu.

Anasema ana amini ana uwezo wa kufunga mabao licha ya ligi kuwa changamoto mbalimbali za kiutendaji akitoa mfano mabadiliko ya mara kwa mara ya ratiba.

Ligi Kuu

Aiyee hafichi hisia zake kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi imeshindwa kujenga mfumo mzuri wa upangaji wa ratiba.

Mchezaji huyo anatoa wito kwa TFF kuweka mfumo bora wa usimamizi wa ligi hasa katika upangaji wa ratiba ili kuboresha mashindano.

Aiyee aliyeanza kucheza soka mwaka 2010 Bambino ya Tanga kabla ya kujiunga na Mwadui mwaka 2011, anamtaja beki wa JKT Tanzania Rahim Juma ‘Zandeni’ ni ‘katili’ anapokuwa uwanjani. Mchezaji huyo anasema wapo mabeki hodari lakini Juma ni beki anayempa taabu timu zao zinapocheza.

Pia Aiyee ametoboa siri ya mafanikio yake ni ‘pacha’ wake Ditram Nchimbi wanaocheza Mwadui. Anasema Nchimbi ndiye mpishi wake wa mabao katika kikosi hicho na amemtaja kuwa ni mchezaji atakayepata mafanikio katika soka.



Chanzo: mwananchi.co.tz