WANAMWITA ‘Bull Striker’ mtambo wa mambo kutoka Yanga Princess ambaye ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu huu .
Jina lake halisi ni Aisha Masaka ambaye amemaliza msimu akiwa amepachika wavuni mabao 35 akimzidi bao moja tu mpinzani wake mkubwa Opah Clement ambaye aliongoza kwa muda mrefu mbio za ufungaji bora kabla ya kuzidiwa mwishoni.
Aisha ambaye ni mrefu kwa umbo mwanzoni mwa msimu alijiwekea malengo ya kufunga mabao 27, lakini uimara wake wa kuzifumania nyavu umemwezesha kumaliza na mabao mengi zaidi huku kati ya mabao 35 akifunga hattrick mara nne.
Lakini jambo lililovutia katika ufungaji wake, amezifunga timu tisa kati ya 11 zilizoshiriki WPL msimu huu na kushindwa kutikisa nyavu za timu mbili tu ambazo ni Simba Queens na Es Unyanyembe.
ES unyanyembe ndio timu pekee ambayo Aisha hakukutana nayo msimu huu kwani kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza hakucheza wakati mchezo wa pili timu hiyo ya Tabora iliingia mitini na kushindwa kutokea uwanjani hivyo kushushwa daraja.
Yanga Princess 4-0 Tanzanite SC
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Novemba 20 mwaka jana Aisha alifunga mabao mawili na kuiongoza timu yake kuichapa Tanzanite (Fountaine Gate) mabao 4-0 huku mabao mengine katika mchezo huo yakifungwa na Amina Ally na Mwantumu Ramadhan.
Yanga Princess 5-0 Baobab Queens
Aisha aliendeleza moto wa kukisaka kiatu cha dhahabu msimu huu baada ya kufunga mabao mawili katika mchezo dhidi ya Baobab Queens uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru Desemba 2 ambao Yanga ilishinda mabao 5-0. Mabao mengine katika mchezo huo yalifungwa na Happiness Mwaipaja, Emiliana Mdimu na Fatuma Makusanya.
Mlandizi Queens 0- 2 Yanga Princess /Yanga 5-1 Mlandizi
AKM10 aliifunga Mlandizi Queens katika mechi zote mbili, akianza mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Desemba 8 mwaka jana kwenye Uwanja wa Mabatini Pwani ambao Yanga ilishinda mabao 2-0 huku Aisha akifunga bao moja na lingine lilifungwa na Fatuma Mwisendi ‘Didier’.
Pia Aisha aliifunga Mlandizi mabao manne alipoingoza timu yake kushinda mabao 5-1 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliofanyika Machi Mosi kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Aniella Uwimana.
Yanga 2-1 Ruvuma Queens /Ruvuma 0- 1 Yanga
Katika mchezo dhidi ya Ruvuma Queens uliofanyika Januari 8 mwaka huu na ambao Yanga Princess ilishinda mabao 2-1, Aisha alifunga bao moja huku lingine likifungwa na Emiliana Mdimu huku pia akiifunga timu hiyo bao moja alipoipa ushindi timu yake wa bao 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa pili uliofanyika Mei 2 kwenye Uwanja wa Majimaji Songea.
Yanga 7-0 Mapinduzi Queens/ Mapinduzi 0- 6 Yanga
Aisha aliifunga Mapinduzi Queens katika michezo yote miwili msimu huu, alianza kwa kuichapa timu hiyo mabao mawili wakati Yanga iliposhinda mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika Januari 11 jijini Dar es Salaam kisha akaitungua mabao manne alipoiongoza timu yake kushinda mabao 6-0 katika mchezo uliochezwa Mei 5.
JKT 0 - 2 Yanga Princess /Yanga 2- 0 JKT Queens
Wajeda nao hawakupona mbele ya Aisha kwani aliwafunga katika mechi zote mbili, akianza kuwachapa bao moja Yanga iliposhinda mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Januari 15 huku pia akiwafunga bao moja alipoiongoza timu yake kushinda mabao 2-0 katika mchezo mwingine uliofanyika Mei 9.
TSC Queens 0 - 7 Yanga Princess / Yanga 7- 0 TSC Queens
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Januari 19 kwenye uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, Aisha alifunga mabao manne na kuiongoza Yanga Princess kuichapa TSC Queens mabao 7-0 huku mabao mengine yakifungwa na Amina Ally na Philomena Kizima.
Katika mchezo wa mzunguko wa pili uliofanyika Mei 17 kwenye uwanja wa Uhuru Aisha alifunga mabao mawili wakati timu yake ilipoibamiza TSC Queens mabao 7-0.
Alliance Girls 0- 5 Yanga Princess
Alliance Girls ndiyo timu iliyofungwa mabao mengi zaidi na Aisha ikiwa imeruhusu mabao saba.
Timu hiyo ilifungwa mabao mawili na mchezaji huyo kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Januari 22 ambao Yanga Princess ilishinda mabao 5-0 pia ilifungwa tena mabao matano na Aisha katika mchezo wa mzunguko wa pili ambao Yanga ilishinda mabao 6-0 uliofanyika Mei 16.
Yanga 3-0 Kigoma Sisterz
Aisha hakuiacha salama timu hii kwania lifunga mabao mawili yanga Princess iliposhinda mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika April 27 kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Bao lingine katika mchezo huo lilifungwa na Aniella Uwimana.