Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Adidas wanampa Geay Sh100 milioni kwa mwaka

Geay Pic Adidas wanampa Geay Sh100 milioni kwa mwaka

Fri, 2 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Jana tuliishia sehemu ambayo Geay alichukua sehemu kubwa ya kuzungumzia kuhusu kiwango cha fedha ambacho alikipata baada ya kushika nafasi ya pili kwenye mbio za Boston.

Alieleza mambo mengi, lakini moja ni kitendo cha kushika shilingi milioni 200 zikiwa ni fedha nyingi ambazo hajawahi kuzishika kwenye maisha yake kwa wakati mmoja.

Lakini alijaribu kuzungumzia kidogo kuhusu bei ya kiatu ambacho alikitumia kwenye mbio hizo, akisema kilikuwa cha shilingi 400,000 lakini alinunua ghali kutokana na aina ya kiatu chenyewe na mastaa ambao wamewahi kukivaa, leo tunaendelea…

Katika sehemu hii, Geay ambaye anatajwa kuwa mwanariadha mahiri zaidi kwa upande wa mbio za Marathoni hapa nchini, anazungumza kuhusu mambo mengi, lakini kubwa ni kuhusu mkataba wake na kampuni kubwa ya Adidas.

“Mimi nina mkataba na Adidas tangu mwaka 2017 nafikiri wengi walikuwa hawafahamu, wamekuwa wakinidhamini kwenye kila kitu ambacho natumia kwenye riadha, wananipa nguo, kama hii niliyovaa, viatu na vitu vingine vingi ambavyo vinanisaidia kwenye kazi yangu, kiuhalisia huwezi kuniona nimevaa nguo ya kampuni nyingine zaidi ya kampuni hii.

“Lakini kumbuka pia wananipa fedha kutokana na mkataba nilionao, ndiyo maana nyuma nilikueleza kuwa niliposhika nafasi ya pili kwenye Boston walinilipa, hiyo ni nje ya mkataba wa mwaka ambao wanatakiwa kunilipa milioni 100 kila mwisho wa mwaka.

“Kila mashindano makubwa ambayo nimekuwa nikikimbia nikishika nafasi tatu za juu wananipa bonasi kutokana na mkataba wangu nao ulivyo, nafikiri nikienda Olimpiki na kupata medali kitakuwa kiwango kikubwa kuliko hiki ninachopata kwa mwaka.

“Hiki ni kiwango ambacho kimekuwa kikinisaidia kufanya mambo yangu mengine ya kimaisha, kimekuwa kikipanda kila mwaka na naamini pia mwakani kitapanda ndiyo maana kiwango ninachoweza kukusanya jumla mwaka huu hakiwezi kuwa sawa na mwakani.

“Ukweli dili zangu nyingine zimekuwa zikitokea kutoka kwa meneja wangu Derick Fraude ambaye anaishi Uingereza, huyu ndiye amekuwa mara nyingi akifuatilia mambo mengi ya mikataba na ishu nyingine kwangu.

“Ukimwambia mtu ni ngumu kuelewa lakini ukweli ni kwamba mimi paspoti yangu imekuwa inajaa kila baada ya miaka mitano kwa kuwa nimekuwa ni mtu wa kusafiri mara kwa mara kwenda nje ya nchi.

TAGETI YAKE KUPATA SH1 BILIONI KWA MWAKA

Geay anasema kila binadamu huwa na tageti zake na mtu mwenye mafanikio ni yule ambaye amekuwa akijiandaa vizuri na kuweka malengo yake kwa siku, wiki, mwezi na hata mwaka. Anasema anaamini kuwa tageti zake za mwaka jana kwenye kipato alichoingiza hakiwezi kuwa sawa na mwaka huu kwa kuwa ameshaweka malengo yake sawa.

“Mwaka jana nilipokuwa nakagua kwenye akaunti yangu niligundua kuwa nimefanikiwa kuingiza milioni 300, hizi ni fedha ambazo ziliingia kutokana na mbio ambazo nilikimbia ndani na nje ya nchi lakini pia ni kutokana na mikataba mingine ukiwemo huu wa Adidas ambao ninao.

“Hivyo hadi sasa naona kuwa mwaka huu kiwango hicho kitapanda kwa kuwa nikiangalia kile ambacho nimeingiza naona ni kikubwa, sijafahamu nitakusanya jumla Sh ngapi, lakini amini kuwa itakuwa zaidi ya hicho cha mwaka jana.

“Tageti yangu ni miaka kadhaa mbele nione nimeingiza Sh1 bilioni kwenye akaunti yangu kwa mwaka, hapa nafikiri kila kitu changu kitakuwa kinaenda sawa, sioni kama itachukua muda mrefu hilo kutimia.

KUHUSU KUMILIKI NYUMBA?

Geay akiwa anazungumza kuhusu nyumba ambazo anamimiliki anasema yeye anapenda kuwa na vitega uchumi, lakini katika maisha yake anapenda kuona anaishi sehemu nzuri, hivyo nyumba kwake ni jambo la muhimu.

Lakini anasema ili uishi vizuri unatakiwa kuhakikisha unakuwa rafiki na watu wanaokunzunguka. Hilo linadhiirika wakati tunapotembea naye kwenye maeneo ya karibu na nyumbani kwake, kwani anaonekana kama mfalme wa mtaa kutokana na kila mtu kumwita kuanzia madreva Bodaboda, bajaji na hata watu wengine wa kawaida na kila sehemu amekuwa akisimama na kuzungumza nao na kuendelea na safari.

“Kwanza elewa kwamba mimi nimetoka Manyara na nyumba zangu za kwanza nilianza kwa kuwajengea wazee wangu kule nyumbani, hizi mara nyingi siziweki kwenye idadi kwa kuwa ni za kwao. “Hapa mjini nina nyumba tatu, siyo nyingi lakini nafikiri baada ya muda nitakuwa nazo zaidi kwa kuwa ni moja ya kitu ambacho napenda kuwa nacho.

“Unajua mara nyingi nyumba ni kati ya kitu ambacho namshauri mtu akiona anaweza kujenga basi afanye hivyo kwa kuwa kwangu ni kitu muhimu kwa maisha ya binadamu,” alisema Geay, huku Mwanaspoti likifanikiwa kuuona mjengo mmoja matata anaomiliki.

KUMBE HANA ISHU YA SIASA

“Mwanzo katika maisha yangu sikuwahi kufikiri kama kuna siku nitakwenda bungeni, unajua kuanzia nilipozaliwa hili halikuwa jambo ambalo nalifikiria, lakini kumbuka mwaka huu nimefika pale hivyo kila mmoja anatakiwa kufahamu kuwa kwenye maisha kuna ndoto zinaweza kutimia.

“Kuhusu siasa, ukweli mimi sina taimu ingawa imekuwa ikizungumzwa hivyo, sijawahi hata kufikiri kuhusu kuwa mbunge kwa kuwa nawaona ni watu wa kawaida kama mimi nilivyo kwa kuwa nimekuwa nikikutana nao mara kwa mara, lakini kwa kuwa hakuna anayefahamu mipango ya Mungu, tusubiri huko mbele tuone itakavyokuwa.

ANASAIDIA WANARIADHA WATANO

Geay anasema pamoja na mambo mengine anafurahi kuona wanariadha chipukizi wanafanikiwa kwani naye kuna watu walifanya kazi kubwa kuhakikisha anafika hapo alipo leo ndiyo maana ana watu nyuma yake ambao anawasaidia kufikia malengo yao.

“Unaona hapa kuna wanariadha watano wale ambao nilikuwa nakimbia nao, hawa ni vijana wangu kila siku nipo nao nawasimamia ili kuhakisha wanatimiza malengo yao.

“Mimi ndiyo nafahamu kuhusu safari zao kama kuna sehemu wanatakiwa kwenda, lakini nawasaidia kwenye mbio mbalimbali za ndani kuhakikisha wamekwenda na kuishi vizuri kwenye mikoa hiyo, mfano ni Tulia Marathoni ambayo ilifanyika hivi karibuni Mkoani Mbeya kuna baadhi walienda na walifanya vizuri baadaye naamini watakuwa wanariadha wakubwa.

USHAURI CHAMA CHA RIADHA

Geay anasema kwake anaona chama cha Riadha Tanzania RT kinafanya kazi nzuri, ingawa wanaweza kufanya zaidi ya hapo ili kuufanya mchezo huu hapa nchini uwe mahiri zaidi.

“Hawa ndiyo wanasimamia riadha, wanafanya kazi nzuri lakini kwangu wanatakiwa kufanya zaidi ya hapa, pamoja nao pia wadau wana kazi kubwa ya kufanya kwani RT hawawezi wenyewe. “Ifike wakati kila mmoja aone ana jukumu la kusaidia mchezo huu kwani hapo tunaweza kufanya mambo makubwa.

Chanzo: Mwanaspoti