Kiungo mkabaji wa zamani wa AC Milan, Gennaro Gattuso hakujiona mchezaji mbele ya mwanasoka bora wa Italia kwa miaka mitatu mfululizo, Andrea Pirlo.
Ufundi wa Pirlo ulimfanya Gattuso kutokwa na maneno hayo na kusema kama asingekuwa kwenye mipango ya makocha kadhaa ambao amepita mikononi mwao angejihusisha na shughuli za uvuvi wa samaki.
Gattuso ambaye alisifika kwa soka la kibabe huku akijipatia umaarufu mkubwa kwa matukio yake ya utata anaamini Pirlo ni miongoni mwa viungo bora waliowahi kutokea kwenye uso wa Dunia.
Wakati akiamini hivyo Gattuso, Kiungo wa Kitanzania, Khamis Abdallah wa Bandari ya Mombasa, Kenya amemtaja mkata umeme huyo kuwa ni miongoni mwa wachezaji aliokuwa akivutiwa nao.
Abdallah ambaye ni kiungo mkabaji anasema alikuwa akivutiwa na morali ya upambanaji wa Gattuso ambaye hakuwa anapenda kushindwa na alionyesha ubora wake kila alipokuwa akipata nafasi ya kucheza kabla ya mwili wake kuchoka.
“Tunacheza nafasi moja na kipindi ambacho nilikuwa nachipukia nilikuwa nikijivunza vingi kutoka kwake ikiwemo ubabe, niliweza kuwaonea vijana wenzangu, lakini baadaye niliamua kubadilika na kuanza kucheza soka la utaratibu maana nilikuwa na ubabe ambao ulipitiliza hadi tukawa tunapigana,” anasema Abdallah.
Kiungo huyo wa Kitanzania ambaye alianza kucheza soka la mtaani Tarime, anasema haikuwa kazi nyepesi kwake kupata nafasi ya kucheza nje ya Tanzania.
“Timu yangu ya kwanza kuichezea ilikuwa Tarime United na baada ya hiyo nakajiunga na Polisi Mara (Sasa Biashara) kwa mkataba wa miezi sita kisha nikaenda Stand United ambayo nilicheza na kuwa sehemu ya wachezaji ambao tulipambana na kuipandisha daraja.
“Nilicheza Stand kwa makubaliano ya kunisomesha chuo maana kipindi hicho nilihitaji kujiendelea kwa kusomea inshu zinazohusu madini, tulipomalizana niliamua kwenda Kenya kwa ajili ya kucheki upatikanaji wa ajira.
“Nilichopanga hakikwenda kama nilivyotaka na badala yake niliamua kugeukia tena soka kwa kutafuta timu ya kuichezea, niliangaika sana na mwishowe nikapata timu ya daraja la kwanza,” anasema Abdallah.
Timu hiyo ya daraja la Kwanza Kenya ambayo alijiunga nayo Abdallah ni Muhoroni ambapo ilikuwa 2015 na akiwa timu hiyo kiungo huyo anasema alijipatia mafanikio ya kutwaa Kombe la top 8 mbele Gor Mahia.
Abdallah anasema alitwaa ubingwa wake wa kwanza Kenya akiwa kama nahodha wa Muhoroni na mara baada ya mashindano hayo alipata dili la kujikunga na Sony Sugar ambayo ilikuwa inashiriki Ligi Kuu nchini humo.
Baada ya kutua Sony Sugar, Abdallah anasema iliingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
“Nikiwa Sony Sugar nilipata bahati ya kuitwa Taifa Stars na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki ikiwemo dhidi ya Botswana, Malawi, Benin na pia nilicheza machuano ya Cecafa nchini Kenya japo matokeo hayakuwa mazuri kwa upande wetu.
“Baada ya mashindano yale niliendelea na majuku yangu ya kawaida ya kuichezea Sony Sugar huku nikijiwekea mikakati ya kutaka kuihama klabu hiyo ili nijiunge na timu kubwa zaidi ambayo itakuwa kwenye mbio za kuwania mataji,” anasema.
Mkataba wake ulivyomalizika kipindi kilichopita cha usajili, Abdallah anasema hakuwa na sababu za kujiuliza mbele ya ofa ya Bandari FC japo awali AFC Leopards ndiyo waliokuwa wa kwanza kuonyesha nia ya kumhitaji.
“Hitaji langu ni kushinda kombe la ligi ya Kenya na nimejiunga na Bandari kwa sababu ni moja ya timu ambayo inamikakati ya kutwaa ubingwa karibu kwenye kila msimu,” anasema Abdallah.
Abdallah angekuwa Gattuso yule ambaye alimpiga pini Ronaldo wa moto kipindi hicho damu inachemka akiwa na Manchester United, Mei 2, 2007 katika mchezo wa raundi la pili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, angewaza kugeukia inshu zake za madini kila akimuona Pirlo.
Gattuso ambaye kwa sasa ni kocha wa AC Milan aliwahi kupewa kadi nyekundu na Nikolaj Hänni Desemba 2, 2012 pindi akiichezea Controversies ya Uswizi kilichotokea kiungo huyo akaichukua na yeye akamwonyesha mwamuzi.
Huyo ndiye Gattuso ambaye Abdallah aliiga utukutu wake alipokuwa akichipukia kwenye soka la mtaani na miongoni mwa athari ambazo alikumbana nayo ni kugomba na wachezaji wenzake ambao alikuwa akicheza nao.