Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

AFCON U-17 Ishara njema ya Serengeti Boys, utaipenda tu

Mon, 24 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ilipotolewa kwenye nusu fainali ya michuano ya Cecafa-CAF U-17 mashabiki wa soka ni wazi walianza kuikatia tamaa kwamba imepoteza kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki ambao una timu laini na haiwezi kufika mbali itakapokuwa mwenyeji mwakani.

Katika mechi zile, Serengeti Boys ilifungwa mabao 3-1 na Uganda nusu fainali na kumaliza ndoto za Tanzania kucheza fainali. Mungu bariki yenyewe ndiyo mwenyeji kwani hata tiketi ilishakosekana.

Hata hivyo, sura ya wachezaji wa Serengeti Boys ilikuwa imejaa bashasha kuwa walikuwa na shauku ya kufika mbali katika michuano ya U-17 ambayo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa na ule wa Azam Complex kule Chamazi, Dar es Salaam.

Serengeti Boys ambayo ilikwenda Botswana kimkandamkanda kwenye michuano ya U-17 ya Cosafa kama timu alikwa, ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo baada ya kuibandua Angola kwa penalti 6-5 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 dakika 90 za kawaida.

Timu hiyo ilitua Botswana na kufungwa mabao 2-0 na Angola mchezo wa kwanza, lakini ikaifunga Afrika Kusini, Zambia kabla ya kuingia fainali na kutwaa ubingwa.

Kwa mujibu wa mtandao wa Cosafa, Tanzania ilitwaa ubingwa baada ya kuonyesha soka la maana, kwani walionyesha wachezaji wake kuwa na vipaji. Mtandao huo ulisema kuwa mchezo ulianza kwa kasi kila mmoja kutaka mabao ya mapema, lakini Tanzania ndiyo iliyotawala sehemu kubwa ya mchezo ikiingia mara nyingi katika 18 za Angola na kusababisha hatari nyingi.

Hata hivyo, Angola ilikuwa ya kwanza kufunga kupitia kwa Gasper Morais dakima tano kabla ya mapumziko na iliichukua Serengeti Boys dakika 16 kusawazisha kupitia kwa Kelvin Pius aliyesawazisha bao safi.

Mengi awatoa

Akizungumza katika hafla ya kuwapongeza, mlezi wao, Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi aliwapa zawadi ya fedha nyota hao kama pongezi za kutwaa ubingwa wa mashindano ya vijana wa umri kwa kanda Kusini mwa Afrika.

Mengi ambaye ndiye mlezi wa timu hiyo, alisema kuwa ameamua kutoa fedha hizo japo hakutaka kuweka hadharani kiwango chake.

“Vijana hawa wamefanya kazi kubwa na nimeona niwape kiasi kidogo cha fedha kama motisha kwao lakini naamini mambo mazuri zaidi yanakuja,” alisema Mengi.

Waziri Mwakyembe atoa neno

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alimpongeza Mengi kwa jinsi anavyoisaidia timu hiyo kama mlezi wake.

“Nakushukuru na nakupongeza sana mzee wetu Mengi kwani tukio hili ni la kihistoria,” anasema Waziri Mwakyembe.

Katika hafla hiyo, Waziri Mwakyembe aliitaka TFF kutengeneza utaratibu wa wachezaji vijana ambao ndiyo muumini wake, kupata namba katika klabu ama za Ligi Kuu au Daraja la Kwanza ili kuwa na mwendelezo wake.

DK Msolla atoa neno

Akizungumzia suala la vijana, kocha mkongwe, Dk Mshindo Msolla anasema: “TFF iwe na kitengo imara cha kuendeleza soka la vijana kwani katika kipindi kirefu ambacho kitengo hicho kipo, hajaona kama kuna dhamira ya ukweli katika maendeleo ya soka kwa vijana.

“Ninakumbuka TFF chini ya Rais Leodegar Chilla Tenga iliwahi kuandaa mpango mkakati wa namna ya kuendeleza soka letu kwa kuanza na vijana na matarajio yetu yalikuwa ni kwamba kurugenzi hiyo ingetumia andiko hilo kama rejea na kuboresha maeneo ambayo yatahitaji kufanyiwa hivyo.

Dk Msolla kama alivyosema Waziri, amepigilia msumari akisema: “TFF iandae mikataba na klabu ambazo zitawachukua wachezaji hao kwa kuwa TFF kama TFF haiwezi muda wote kuwa na uwezo wa kuwatunza wachezaji hao, bali klabu ndizo zenye jukumu hilo.

Anasema Kutokana na ukweli huo, wachezaji wengi huchukuliwa na klabu za madaraja mbalimbali lakini anasema jambo linalosikitisha ni kwamba wengi wa wachezaji hao hujiunga na vilabu hivyo bila ya usimamizi wa maana kutokana na ukweli kwamba wengi hawana mameneja wenye weledi.

Yatajiwa wababe wake

Baada ya furaha ya ubingwa wa Cosafa, Serengeti Boys inatakiwa kuonyesha kile ilichofanya kwenye michuano hiyo itakapokuwa hapa nchini kuanzia Aprili 14 hadi 28.

Serengeti Boys imepangwa Kundi A pamoja na mabingwa wa Cecafa, Uganda, mabingwa wa Ukanda wa Wafu Kanda B – Afrika Magharibi, Nigeria ambao ndio Serengeti Boys inaanza nao mechi ya ufunguzi.

Timu nyingine ya kundi hilo ni Angola ambao ndio mabingwa wa Cosafa. Angola wameshafahamu makali yao, waliwafunga mabao 2-0 mechi ya kwanza michuano ya juzi kabla ya kuwafunga tena fainali kwa penalty 6-5.

Mabingwa hao wa Cosafa wenyewe wataanza na Uganda.

Kundi B la michuano hiyo linaundwa na Guinea, Cameroon, Senegal na Morocco. Mechi ya ufunguzi itakuwa kati ya Guinea na Cameroon na kufuatia mchezo wa Morocco na Senegal.

Hata hivyo, fainali hizo za Afrika kwa vijana, zitafanyika bila ya uwepo wa timu tatu kati ya nne ambazo zilifuzu nusu fainali ya mashindano hayo mwaka jana zilizofanyika Gabon ambazo ni bingwa, Mali, washindi wa pili, Ghana na Niger walioshika nafasi ya nne

Droo ya upangaji wa makundi ya mashindano hayo, ilifanyika Alhamisi iliyopita kwenye Ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa soka nchini.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA), Injinia Moses Magogo ndiye aliyeongoza ujumbe wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) uliokuja nchini kusimamia na kuongoza droo hiyo.

Washindi wawili wa kila kundi hilo watafuzu hatua ya nusu fainali ambayo pia inawawezesha kushiriki fainali za Kombe la Dunia kwa vijana zitakazofanyika nchini Peru mwakani.

Kocha wa Serengeti Boys

Akizungumzia ratiba hiyo, kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo anasema kuwa mpango wake ni kushinda mechi mbili za kwanza na hata zote kwani hataki kupigia wengine hesabu ili kusonga mbele. “Tumeshaanza maandalizi na yoyote atakayekuja mbele yetu hatuwaogopi japokuwa timu zote ni nzuri,” anasema.

Anasema kuwa maandalizi yamekamilika na kila hatua inaendelea kufanyiwa kazi.

“Tuna program nyingi za maandalizi na ninaamini timu itakapokwenda Uturuki itakuwa imejikamilisha kwani kule tutacheza mechi nyingi za maandalizi na kutengeneza timu imara.”

Milambo alisema kuwa wanaendelea na mazoezi lakini kwa sasa anakiamini kikosi chake na timu yake iko tayari kucheza na yoyote kwa zaidi na zaidi anachotaka kuangalia ni kiwango na si matokeo.

Wapinzani wa Serengeti Boys

Nigeria

Vijana wa Nigeria wanatarajiwa kuwa wapinzani wakuu wa Serengeti Boys kwenye kundi lao la A, kutokana na kiwango cha timu hiyo ambayo ngazi yao ya vijana chini ya umri wa miaka 17, wamewahi kushiriki Fainali za Kombe la Dunia.

Tanzania itaanza na Nigeria ambayo ilipata tiketi ya kushiriki fainali hizo kwa kuitandika Ghana kwenye fainali ya ukanda wao wa Magharibi B.

Angola

Tanzania ilicheza na Angola kwenye Fainali za Afcon za Gabon mwaka jana na Serengeti Boys kushinda mabao 2-1. Mbali na Nigeria, Angola ni wapinzani wengine wa Serengeti Boys ambao wanatarajiwa kuleta ushindani kwenye kundi hilo.

Wiki iliyopita, walikutana kwenye michuano ya Cosafa ya U-17 na Angola ilishinda mabao 2-0 mchezo wa kwanza kabla ya kukutana tena fainali na kutoka sare ya 1-1 na Tanzania kuilaza Angola penalti 6-5.

Uganda

Majirani Tanzania na Uganda wako kundi moja na mara mwisho kukutana ilikuwa Agosti 24 mwaka huu na kwenye mchezo huo Serengeti Boys ilipoteza kwa mabao 3-1.

Ilikuwa mechi ya nusu fainali ya Cecafa-CAF U-17 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.



Chanzo: mwananchi.co.tz