Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakuu wa nchi Sadc wakubaliana mambo haya

Video Archive
Mon, 19 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), John Magufuli ambaye ni rais wa Tanzania ametaja mambo kadhaa yaliyopitishwa katika kikao cha wakuu wa nchi 16 za jumuiya hiyo kilichofanyika jana Jumamosi Agosti 17, 2019 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza leo Jumapili Agosti 18, 2019 kabla ya kuhitimishwa kwa kilele cha mkutano wa wakuu wa nchi hizo,  Rais Magufuli amesema wameagiza Sekretarieti kuanzisha chombo cha kukabiliana na majanga ili kuzisaidia nchi wanachama zitakapokumbwa na mafuriko, njaa na magonjwa ya milipuko.

Mkutano wa wakuu wa nchi umefanyika jana na leo na ulitanguliwa na maonyesho ya bidhaa katika wiki ya viwanda yaliyoanza Agosti 5 hadi 8, 2019 na baadaye ikafuata mikutano ya kamati ya watalaam pamoja na baraza la mawaziri wa Sadc.

“Kwanza wakuu wa nchi wamewapongeza viongozi waliomaliza muda wao kutumikia Sadc, walipitia hali ya uchumi na kuangalia changamoto ya majanga,” amesema Rais Magufuli.

Amesema jambo jingine wameagiza Burundi iliyoomba kuwa mwanachama wa jumuiya hiyo kukamilisha hatua kadhaa kwa kuwa kuna baadhi ya vitu hawajakamilisha.

Magufuli amesema wakuu hao pia wamekubaliana kila nchi mwanachama kuendelea kuhimiza utekelezaji wa  mkakati wa viwanda 2015/63 katika nchi husika ili kufikia malengo.

Habari zinazohusiana na hii

Pia, wakuu hao wamekubaliana kuhakikisha kila nchi inaendelea kutilia mkazo uwekezaji wa miundombinu kwa kuwa ndio chanzo cha kufanikisha mkakati wa viwanda na uchumi wa Sadc.

Nchi hizo pia zimekubaliana kuimarisha mazingira ya taasisi za kifedha.

Magufuli amesema kikao hicho pia kimepitisha mpango wa kuongeza mapato ya Sadc, kila nchi itaangalia namna ya ushiriki katika uchangiaji.

Chanzo: mwananchi.co.tz