Dar es Salaam. Baadhi ya wanachama wa Chadema waliopo nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kufuatilia kesi inayowakabili viongozi wanane wa chama hicho wameanza kukamatwa na polisi.
Hukumu ya kesi hiyo imeanza kusomwa leo Jumanne Machi 10, 2020 saa 7:15 mchana na Hakimu Mkazi mkuu wa Mahakamani ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba huku ulinzi ukiwa umeimarishwa ndani, nje ya mahakama hiyo.
Mwananchi limeshuhudia nje ya mahakama hiyo polisi wakiwataka wanachama hao kutulia na baada ya muda kuanza kuwakamata mmoja baada ya mwingine.
Awali, wanachama hao walikuwa katika viwanja vya mahakama baada ya kutakiwa kutoka ndani ya chumba cha mahakama kutokana na wingi wao.
Walipokuwa nje polisi waliwataka kukaa kimya lakini wapo waliotii amri hiyo na wengine kupinga huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kulituhumu Jeshi la Polisi.
Baada ya muda walitolewa nje ya uzio wa mahakama hiyo, kutakiwa kuwa watulivu eneo ambalo polisi wamewakamata.
Habari zinazohusiana na hii
- Picha ya hukumu ya kina Mbowe kortini leo
- Hukumu kesi ya kina Mbowe yaanza kusomwa
- VIDEO: Hukumu kesi ya kina Mbowe saa saba, ulinzi waimarishwa
Katika kesi hiyo namba 112 ya mwaka 2018 washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 13 ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali kati ya Februari 1 na 16, 2018.
Viongozi mbalimbali wa Chadema wakiwemo wabunge na wenyeviti wa kanda ni miongoni mwa waliojitokeza kusikiliza hukumu hiyo.
Wengine ni kutoka vyama vingine vya upinzani akiwemo mshauri mkuu wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad.
Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.
Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika; naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Esther Matiko (Tarime Mjini); Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda) na John Heche (Tarime Vijijini).