Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania imeomba Bunge kuongeza idadi ya wabunge watakaochangia taarifa za kamati za chombo hicho cha Dola zilizowasilishwa bungeni leo Jumanne Februari 4, 2020.
Leo wabunge wanajadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati tatu za utawala na Serikali za mitaa, katiba na sheria pamoja na sheria ndogo.
Akiomba mwongozo wa Spika bungeni leo mnadhimu wa Kambi Rasmi ya upinzani bungeni, Ester Bulaya amesema hawawezi kuwanyima wabunge hasa wa upinzani kutoa maoni yao kwa kamati muhimu kwa sababu ya kisingizio cha muda.
“Kwa mujibu wa kanuni zetu za Bunge kiti chako kinaweza kuongeza muda hadi pale shughuli zitakapokamilika. Mwenyekiti hatuwezi kuwanyima wabunge hasa Kambi Rasmi ya Bungeni kutoa maoni yao katika kamati muhimu za leo,” amesema.
Amesema wanaomba wapewe nafasi za nyongeza za kuchangia ili wabunge wapate nafasi za kutoa maoni yao.
“Tunajadili kamati mbili upande wa Chadema tunapata, CUF wanapata nafasi ya ziada, leo tunajadili kamati tatu mnatoa CUF nafasi moja na Chadema nafasi mbili,” amesema.
Pia Soma
- Wawili mbaroni kwa kusafirisha Heroin
- Wakili ataja makosa ya Mwamposa na wenzake
- Mkemia kuchunguza vifo vya wanajeshi 10
Akijibu suala hilo mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga amesema ratiba za Bunge zinaenda kwa mujibu wa utaratibu na kwamba ratiba yao ya leo nafasi za Chadema ni mbili na CUF ni moja.
“Kwa hiyo kama mnataka kuchangia zaidi mgawane dakika kazi itakwenda,” amesema Najma na kuruhusu kuendelea na shughuli zilizopangwa.