Dar es Salaam. Jeshi la Uokoaji na Zimamoto nchini Tanzania limewataka wakazi wa jijini Dar es Salaam kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali.
Limesema kwa wananchi watakaopata athari zaidi ikiwa ni pamoja na kuzingirwa na maji katika maeneo hatarishi wapige namba 114 kwa ajili ya kupewa msaada.
Tahadhari hiyo inatolewa na jeshi hilo katika gari linalopita mitaani kueleza hali ilivyo tangu mvua hiyo ilipoanza kunyesha leo asubuhi Jumanne Desemba 17, 2019.
Limewataka wananchi wanaoishi mabondeni kuhama ili wasipate madhara zaidi.
Akizungumza na Mwananchi leo ofisa operesheni wa jeshi hilo, Isack Njombe amesema mvua zimeleta athari na baadhi ya maeneo kutopitika kutokana na barabara kufungwa.
“Tunawatangazia kuwa hali sio nzuri mvua hizi ni kubwa wanaoishi mabondeni ni vizuri wakahama kwa tahadhari.”
“Ikitokea umezingirwa na maji na kuna hatari tunaomba watupigie simu kwa namba 114 ili tuweze kutoa msaada, watambue kuwa jeshi la zimamoto liko kwa ajili yao,” amesema Njombe