Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Serikali ya Tanzania yampa pole Erick Kabendera kufiwa na mama yake, yapinga kwenda kumuaga

Video Archive
Thu, 2 Jan 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari nchini Tanzaniua, Erick Kabendera umempa pole, baada ya kufiwa na mama yake mzazi, Verdiana Mujwahuzi.

Mbali na kumpa pole, Serikali ya Tanzania imepinga maombi ya upande wa utetezi  ya kutaka mshtakiwa huyo aruhusiwe kesho Ijumaa Januari 3, 2020 kwenda kushiriki Ibada ya mazishi ya mama yake katika Kanisa Katoliki la Chang'ombe, jijini Dar es Salaam.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka matatu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kukwepa kodi na kutakatisha zaidi ya Sh.173 Milioni katika kesi ya uhujumu namba 75/2019.

Leo Alhamisi, Januari 2, 2020 Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon ametoa pole hizo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Simon aliieleza Mahakamani hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega kuwa Serikali ya Tanzania inampa pole Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi.

"Hata sisi tuna masikitiko makubwa na tunampa pole nyingi Kabendera kwa kufiwa na mama yake mzazi, lakini mahakama isifungwe mikono kwa maombi yaliyowasilishwa ya kutaka mshtakiwa kushiriki msiba," amedia  Wankyo.

Akijibu hoja za upande wa utetezi, Wankyo amedai maombi ya Kabendera kupitia mawakili wake yamewasilishwa wakati ambao si sahihi kwa sababu mahakama haina mamlaka na pia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hajaipa kibali mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.

"Mheshimiwa hakimu katika macho ya kisheria mahakama yako haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa sababu kesi hii ni ya uhujumu uchumi, licha ya kuwa hata sisi tuna masikitiko makubwa lakini tunaiomba mahakama yako isifungwe mikono," amedai

Awali, Jebra Kambole aliwasilisha mahakama ombi la kuiomba mahakama ya Kisutu imruhusu Kabendera akashiriki ibada ya kumuaga mama yake mzazi katika Kanisa la Roman Katoliki lilipo Changombe, wilaya ya Temeke majira ya mchana, huku akiwa chini ya ulinzi.

Kambole ameieleza mahakama kuwa suala la kushiriki sala ya mwisho ya msiba ni haki ya msingi ya binadamu na ni haki ya faragha na ni haki ya kuheshimu familia.

"Kushindwa kuhudhuria maziko ya mama yake tutakuwa tumemuadhibu adhabu kubwa tena kwa kuangalia uhusiano wa mshitakiwa na mama yake mzazi kwani alikuwa akimuuguza na ni vizuri akatoa heshima ya mwisho," amedai Kambole.

Amedai ni muhimu kwa Kabendera kushiriki ibada ya kumuaga mama yake mzazi kwa sababu mama mzazi ni mmoja, akifa anaagwa mara moja na kama kumzika anazikwa mara moja.

"Hivyo ni muhimu mshtakiwa akahudhuria tukio hili la kibinadamu," amedai Kambole na kuongezea

"Jamhuri haitaathirika kwa lolote kwa sababu mshitakiwa atakuwa chini ya ulinzi na ibada itakuwa mchana kanisani na Temeke sio mbali na gerezani, tunaomba akatoe heshima ya mwisho," ameomba.

Baada ya kutoa hoja hizo, Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi kwa muda hadi saa 8:45 mchana wa leo Alhamisi, ambapo atatoa uamuzi kama Kabendera ashiriki Ibada ya mazishi ya mama yake mzazi au laa.

Mama wa Kabendera alifariki dunia Jumanne ya wiki hii Desemba 31, 2019 katika Hospitali ya Rufaa ya Amana jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa siku mbili kwa ajili ya matibabu.

Chanzo: mwananchi.co.tz