Unguja/Dar. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein jana alikagua gwaride la mwisho akiwa Rais wa visiwa hivyo katika sherehe za maadhimisho ya Mapinduzi.
Katika maadhimisho ya mwakani, Zanzibar itakuwa na Rais mwingine kwa sababu Dk Shein anamaliza vipindi vyake viwili vya miaka mitano mitano Novemba mwaka huu.
Safari ya urais wa Dk Shein ilianza Oktoba 31, 2010 aliposhinda uchaguzi na kuapishwa rasmi Novemba 3, 2010 kama Rais wa Saba wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Jana, Dk Shein alikagua gwaride hilo lililoenda sambamba na kupigiwa mizinga 21 wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Uwanja wa Amaan.
Viongozi mbalimbali walihudhuria maadhimisho hayo akiwemo Rais wa Tanzania, John Magufuli, makamu wake, Samia Suluhu Hassan, makamu wa pili wa rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Pia, marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume walihudhuria.
Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa, Frederick Sumaye na Mizengo Pinda nao walihudhuria sherehe hizo.
Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma na Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omary Othman Makungu na wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama.
Katika sherehe hizo, Rais Shein aliwasili uwanjani hapo akitumia gari maalumu la wazi na akazunguka nalo uwanjani kusalimiana na mamia ya wananchi waliojitokeza.
Kisha alifika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya wimbo wa Taifa la Zanzibar na Jumuiya ya Afrika Mashariki uliokwenda sambamba na kupigiwa mizinga 21.
Baadaye Rais Shein alipokea maandamano ya wananchi kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar yakihusisha wafanyakazi wa taasisi mbalimbali za Serikali pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Baadhi ya waandamanaji hao waliojawa na bashasha walipita mbele ya jukwaa kuu wakiimba nyimbo za hamasa zilizobeba kauli mbiu ya mapinduzi daima ‘’tutayalinda na kuyatunza potelea mbali’.
Katika hotuba yake aliyolazimika kuikatisha kwa madai ya uwepo wa jua kali uwanjani hapo, Rais Shein alisema maslahi ya watumishi wa umma yameongezeka kutoka Sh83.1 bilioni mwaka 2010/11 hadi kufikia Sh417.9 bilioni mwaka 2018/19 sawa na ongezeko la mara 5.1.
Alisema mafanikio yote yametokana na kasi ya ukuaji wa uchumi visiwani hapa na kwamba hiyo imesaidia wafanyakazi kulipwa mishahara kwa wakati.
Katika hatua nyingine alisema watumishi wa umma wastaafu malipo yao ya pensheni yameongezeka kutoka Sh25,000 kwa mwezi kwa mwaka 2017 na kufikia Sh90,000 kwa mwezi, mwaka 2019.
Aliahidi kuwa kabla ya kumaliza muda wake anafikiria kuongeza mishahara kwa wafanyakazi kwa kuwa mazingira ya kufanya hivyo yapo.
Kuhusu amani na utulivu visiwani hapa, Rais Shein alisema ili iendelee kubaki, kila mtu anapaswa kufahamu kuwa suala hilo ni jukumu la kila mmoja.
‘’Suala la amani halina mbadala hivyo kila mmoja anapaswa kukataa kuichafua amani na kuhakikisha anashirikiana na Serikali kwa lengo la kuitunza na kuienzi,’’ aliongezea.
Utumishi wake serikalini
Alisema kuna mafanikio makubwa tangu Serikali yake ilipoingia madarakani ikiwemo utekelezaji mkubwa wa mipango kama Mkuza (Mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini Zanzibar) kutoka awamu ya kwanza hadi ya tatu.
Pia alisema amefanya juhudi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha uchumi na kusababisha kuongezeka kwa pato halisi la Taifa kwa mara 1.6 zaidi kutoka thamani ya bilioni 1,768 kwa mwaka 2010.
Msamaha kwa wafungwa
Rais Shein alitumia siku hiyo kutoa msamaha kwa wafungwa 19 ambao bado walikuwa wakiendelea kutumikia makosa yao katika magereza ya Unguja na Pemba.
Taarifa iliyotolewa na katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Abdulhamid Yahya Mzee ilieleza kuwa msamaha huo ulitolewa juzi.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Rais ameridhika kuwa kuna sababu za kutosha za kutumia uwezo wake huo katika sherehe hizo na kuagiza wafungwa hao waachiwe huru.
Msamaha huo ambao hutolewa kila mwaka katika kipindi cha sherehe za Mapinduzi, huwahusisha wafungwa ambao ni wazee sana, wenye maradhi sugu au wenye makosa madogo ambao wamebakiza muda mfupi wa kutumikia kifungo chao.
Wafungwa wenye makosa ya kuua kwa makusudi, wizi wa kutumia nguvu, wizi wa mali ya umma, makosa ya kudhalilisha wanawake na watoto, makosa ya dawa za kulevya hayahusiki na msamaha huo.
Vyama vya ADC na CUF navyo havikuwa nyuma katika maadhimisho hayo kwani baadhi yao walionekana kwenye maandamano yaliyopita uwanjani hapo na kupokelewa na Rais Shein.
Shangwe na nderemo ziliibuka uwanjani hapo baada ya vyama hivyo kupita. Wanachama wa CUF wakiwa mbele na sare zao za chama na bendera walipita.
Nyuma yao walionekana wanachama wa ADC pia wakiwa wamevalia sare na bango lililokitambulisha chama chao.
Sherehe hizo ziliambatana na burudani mbalimbali zilizosisimua wahudhuriaji ikiwemo kwata ya kimya kimya iliyotolewa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Askari hao wapatao 32 wakiwa na viongozi wao wawili walionyesha umahiri wao katika kuchezea bunduki kwa madoido bila kuziangusha.
Wakiwa wenye ukakamavu wameweza kucheza na bunduki hizo wanavyotaka na wakati mwingine hata kurushiana.
Hawakuishia hapo walinogesha zaidi pale walipojipanga mistari na kuzipisha bunduki hizo bila kumgusa kiongozi wao aliyekuwa anapita katikati yao.
Pia onyesho lililofanywa na makomandoo waliovunja matofali na vigae kwa kutumia mikono, kuvutwa na gari na kuruka juu ya gari ilikuwa ni mojawapo ya burudani.