Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mgonjwa wa kwanza nchini kuugua corona apona

Video Archive
Thu, 26 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku tano baada ya Isabela Mwampamba ambaye ni mtu wa kwanza kubainika kuwa na virusi vya corona nchini, Rais John Magufuli amesema vipimo vipya vimeonyesha hana tena maambukizi.

Machi 16, mwaka huu Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitangaza uwepo wa mgonjwa wa kwanza wa corona ambaye aliwasili nchini akitokea Ubelgiji.

Jana akilihutubia Taifa, Rais Magufuli alisema wagonjwa wote waliokutwa na virusi hivyo akiwemo Isabela wanaendelea vizuri na Isabela vipimo vyake vinaonyesha hana tena maambukizi.

“Vipimo vya leo (jana) vilivyochukuliwa kwa watu 20 hakuna aliyekutwa na maambukizi. Hata mgonjwa wetu wa kwanza aliyepatikana kule Arusha naye ni negative (hana maambukizi) nawashukuru madaktari na wauguzi kwa moyo wao wa kujitolea wa kuwahudumia wagonjwa hawa,” alisema kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Isabela (46) aliwasili Tanzania Machi 15 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) akitokea Ubelgiji na alikaguliwa uwanja wa ndege lakini hakugundulika kuwa na homa kuashiria ugonjwa huo.

Baada ya kutoka uwanjani hapo alianza kujisikia vibaya na ndipo alipoamua kwenda hotelini ili kujitenga na familia yake kisha kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu na alipofanyiwa uchunguzi alibainika ana virusi hivyo.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Siku mbili baada ya taarifa hiyo Waziri Ummy alizungumza na Isabela kwa njia ya simu mbele ya mkutano na wanahabari ndipo akatumia fursa hiyo kuomba radhi kwa kile alichodai kwamba anajiona kama chanzo cha kuingia kwa ugonjwa huo nchini.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli hadi sasa Tanzania ina wagonjwa 12 kati ya hao wanne ni raia wa kigeni na wanane Watanzania.

Miongoni mwao ni Isabela, mwanamuziki Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ na meneja wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Sallam Sharaf.

Hadi jana jioni takwimu zilionyesha kuwa watu zaidi ya 315,263 wameshaambukizwa virusi hivyo ulimwenguni kote na kati yao zaidi ya 96,000 wamepona huku kukiwa na vifo vya watu zaidi ya 13,500.

Chanzo: mwananchi.co.tz