Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Membe ana vizingiti 3, Msekwa atia neno

Video Archive
Tue, 3 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukerewe/Dar es Salaam. Wakati katibu mtendaji wa zamani wa CCM, Pius Msekwa akisema kutimuliwa kwa Bernard Membe hakutakuwa na athari, wachambuzi wa siasa wamemwambia mwanasiasa huyo kuwa anakabiliwa na vizingiti katika siku zijazo za maisha yake ya kisiasa.

Membe alitimuliwa wiki iliyopita na CCM kwa makosa ya kuvunja kanuni za maadili huku katibu mkuu mstaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana akipewa karipio kali litakalomzuia kujihusisha na siasa kwa miezi 18, wakati katibu mwingine wa zamani, Yussuf Makamba akisamehewa.

Uamuzi huo ulitangazwa baada ya makada hao kuhojiwa na kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu inayoongozwa na makamu mwenyekiti, Philip Mangula na baadaye Kamati ya Maadili iliyokuwa chini ya mwenyekiti, John Magufuli kabla ya Kamati Kuu kufikia uamuzi wa kutoa adhabu hiyo.

Msekwa atia neno

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalum nyumbani kwake Mtaa wa Nkilizya mjini Nansio, Ukerewe juzi, Msekwa, ambaye pia alikuwa makamu mwenyekiti wa CCM (Bara), alisema chama hicho ni taasisi kubwa yenye mizizi na misingi imara isiyoyumbishwa na wanachama au kiongozi mmojammoja au makundi yanayokinzana na taratibu za chama.

“Membe si wa kwanza kufukuzwa,” alisema Msekwa, ambaye pia alikuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Wapo wengi wamefukuzwa na CCM, wakiwamo wenye madaraka makubwa kama Maalim Seif Sharif Hamad aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

“Tanu ambayo ndiyo imezaa CCM pia imewahi kumfukuza aliyekuwa katibu mtendaji wake wakati huo, marehemu Oscar Kambona alipopingana na maazimio ya Arusha. Huu ni utaratibu wa kawaida wa kikatiba na kanuni kudhibiti nidhamu.”

Akionyesha msisitizo, Msekwa, ambaye pia ni katibu wa baraza la wazee wa chama hicho, alisema, “Kimsingi, hakuna athari kwa makada hawa kuwajibishwa na mwingine kufukuzwa. Ni sawa tu na ambavyo haikutokea athari yoyote viongozi na makada wengine walipofukuzwa siku za nyuma.

Wakati Kambona alienda kuishi ukimbizini nchini Uingereza, Seif alikabiliana na mamlaka na alikuwa mmoja wa waliopigania kurejeshwa kwa siasa za vyama vingi na amekuwa akitoa upinzani mkali katika uchaguzi wa urais wa Zanzibar.

Wakati Msekwa akionyesha kuwa kuondoka kwa Membe hakutayumbisha chama hicho kikongwe, wachambuzi waliohojiwa na gazeti hili wamesema waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje, anakabiliwa na mtihani mzito wa kuvuka vikwazo vitatu iwapo atataka kuendeleza ndoto yake ya urais ambayo amesema “haijafa”.

Membe hajasema safari yake ya kisiasa ya kutimiza ndoto hiyo itaendeleaje, lakini alisema si suala la muda na akadokeza kuwa ana watu serikalini, ndani ya chama na kwingineko.

Kauli yake inadokeza kuwa anaweza kuendeleza ndoto yake ndani ya chama hicho, lakini wachambuzi wanaona safari hiyo ina mabonde na milima.



Walisema Membe anakabiliwa na kikwazo cha kufanya siasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano kupiga marufuku mikusanyiko ya kisiasa na kuruhusu wale waliochaguliwa tu, ambao pia kuna nyakati hukumbana na vyombo vya dola katika maeneo yao.

Walisema hataweza kutumia majukwaa ya kisiasa kuanza kujinadi mapema kwa nafasi hiyo kubwa, au kutumia vyombo vya habari kuwasiliana na wananchi.

“Katika mazingira hayo magumu, Membe anaweza kuwa mwanasiasa wa chini kwa chini akipanga mikakati ya wanasiasa wengine,” alisema Profesa Mohamed Bakari, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Siasa za underground ni pale ambapo haujiungi na chama chochote, lakini katika upangaji wa mikakati ukawa mmoja katika wahusika wakubwa. Mazingira ni magumu, lakini haina maana kuwa huwezi kufanya siasa.”

Kizingiti hicho kilimfanya mwanasiasa mkongwe nchini, Njelu Kasaka amshauri Membe akae kimya.

“Mazingira ya sasa ya siasa si rafiki. Kwa hiyo ata-operate (atafanya siasa) katika mazingira magumu. Kama wanasiasa wa sasa walio kinyume na Serikali wanavyopita katika wakati mgumu basi na yeye atapitia,” alisema Kasaka.

Naye mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mtetezi wa haki za binadamu, Edwin Soko alisema njia ya Membe imejaa miiba ambayo atalazimika kuvumilia ikimchoma, akitaja kuaminiwa na vyama vya upinzani kuwa ni kizingiti kingine kwa mbunge huyo wa zamani wa Mtama.

Alisema Membe ana wakati mgumu wa kuaminiwa na vyama hivyo ambavyo mwaka 2015 vilipokea wanachama wengi kutoka CCM vikawapa fursa ya kugombea uongozi, lakini vikashuhudia wengi wakirejea chama hicho, akiwemo Edward Lowassa aliyepewa fursa ya kukamilisha “safari ya matumaini” kwa kugombea urais.

Mbali na Lowassa, wenyeviti wa mikoa, baadhi ya wabunge na madiwani waliohamia vyama vya upinzani, walikuwa wakitangaza kurejea CCM kwa maelezo kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais Magufuli na wengine wakisema wanashindwa kutekeleza shughuli za maendeleo wakiwa upinzani.

Mtandao wa kumbeba Membe kisiasa

Kizingiti cha pili kwa Membe ni kulazimika kusaka kundi la wanasiasa linalomuunga mkono kama alivyokuwa ndani ya CCM.

Membe aliyejitosa kugombea urais mwaka 2015 alikuwa na kundi lake huku pia akiungwa mkono na makundi mengine ya wasaka urais.

Kufukuzwa kwake ndani ya chama hicho kunamtenga na makada hao ambao wengi wao watakuwa wakihofia kuhusishwa naye ili wabaki salama ndani ya chama hicho. Membe alikuwa pia miongoni mwa wanasiasa waliokuwemo katika kundi la mtandao lililomuingiza Jakaya Kikwete madakarani mwaka 2005.

Akizungumzia kikwazo hicho, Soko alieleza haitakuwa kazi rahisi kwa Membe kusuka mtandao mpya kuweza kukabiliana na CCM.

Soko alisema mtandao uliomuingiza madarakani Kikwete ulifanikiwa kutokana na mambo mawili.

“Mtandao wa Kikwete ulitokana na makada wa CCM, ambao walikuwa wasomi kama Membe walioandaa mikakati na pia kulikuwa kuna kundi kubwa la wafanyabiashara wenye fedha nyingi waliogharamia kampeni hiyo,” alisema Soko.

Soko alisema jambo hilo litakuwa gumu kwa Membe kuweza kukusanya watu wa aina hiyo na hasa ukizingatia yupo nje ya CCM.

“Itakuwa kazi sana kwa Membe kupata wasomi na wafanyabiashara wakubwa wa kumsaidia na hasa ukizingatia yupo nje ya CCM. Ni ngumu sana kwa mtu kujitokeza kupambana na mfumo wa dola kwa sasa ukizingatia Rais aliyepo anawania kipindi cha pili,” aliongeza Soko.

Kuwania urais dhidi ya Rais

Kizingiti cha tatu cha Membe kutekeleza ndoto yake ni kuonyesha nia ya kupambana na rais anayetetea kiti chake kwa awamu ya pili.

Kiutamaduni, Rais John Magufuli anatakiwa kuwa mgombea pekee wa CCM ili atetee kiti hicho mwaka huu.

Wakati Augustine Mrema alipojiunga na upinzani na kugombea urais mwaka 1995 na Edward Lowassa alipofuata nyayo mwaka 2015, waliitikisa CCM.

Hata hivyo, waliingia katika muda mabao marais waliokuwa madarakani walikuwa wanamaliza muda wao. Ali Hassan Mwinyi alikuwa anamalizia awamu ya pili mwaka 1995 wakati Kikwete alikuwa anafikia ukingoni 2015.

Hata hivyo, kwa Membe ni tofauti kwa kuwa hata akiungwa mkono na wanachama kama ilivyokuwa kwa Lowassa mwaka 2015, hataweza kumkabili mwenyekiti wake.

“CCM si chama, ni sawa na dola. Kwa hiyo nguvu kubwa ya chama hicho si tu inatokana na wanachama, bali pia inatokana na nguvu ya dola. Mnaweza mkafukuza wanachama wengi na viongozi wengi na msiathirike kwa sababu nguvu kubwa inayotumika ni nguvu ya dola,” alieleza.

Chanzo: mwananchi.co.tz