Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mashtaka wabunge Chadema haya hapa, wapata dhamana

Video Archive
Thu, 26 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam . Wabunge watatu wa Chadema, Boniface Jacob ambaye ni meya wa Ubungo na diwani wa Tabata, Patrick Asenga na watu wengine 11 wameachiwa kwa dhamana baada ya kufikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka saba yanayowakabili.

Kati ya mashtaka hayo yapo ya kufanya mkusanyiko, kutotii amri halali katika geti la gereza la Segerea jijini Dar es Salaam na kufanya uharibifu katika geti hilo.

Wabunge hao ni Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda) na Jesca Kishoa (Viti Maalumu). Pia yupo mfanyabiashara Henry Kilewo ambaye ni katibu wa Chadema Kanda Kuu ya Dar es Salaam.

Washtakiwa hao wapo 27 lakini waliofikishwa mahakamani leo ni 15 huku chombo hicho cha Dola kikitoa hati ya wito wa washtakiwa 12  ambao leo hawakufika mahakamani hapo.

Wamesomewa mashtaka  na jopo la mawakili watatu wa Serikali  ambao ni, Renatus Mkude, Mkunde Mshanga na Ester Martine.

Wamedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 61/2020.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, wakili Mkude amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kutotii amri halali iliyotolewa na askari Magereza.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Machi 13,  2020 katika gereza hilo lililopo wilayani Ilala kwamba kwa makusudi walikaidi amri halali ya kuondoka eneo hilo kwa amani.

Amesema amri hiyo ilitolewa na askari mwenye namba B 3648, sajenti John ambaye ni mlinzi wa geti hilo.

Katika shtaka pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko, washtakiwa wanadaiwa walikusanyika  isivyo halali na kusababisha hofu ambayo ingeweza kusababisha  uvunjifu wa amani na utulivu.

Shtaka la tatu ni kufanya uharibifu katika gereza ambalo linawakabili washtakiwa wote.

Mshanga amedai  washtakiwa  waliharibu geti kuu la kuingilia na kutokea katika gereza la Segerea ambalo ni mali ya Serikali ya Tanzania.

Katika shtaka la nne  linalomkabili Mdee pekee anadaiwa siku hiyo kutoa lugha ya kuudhi.

Wakili Mshanga amedai Mdee alitoa maneno ya kuudhi kwa sajenti John na kunukuu maneno hayo, “m...., kibaraka wa CCM unakaa nyumba za bati mshahara Sh70,000 wewe sajenti, sajenti fungua geti wewe.”

Amesema maneno hayo yalisababisha uvunjifu wa amani.

Katika shtaka la tano linalomkabili Bulaya, wakili Mshanga amesema mbunge huyo alitoa lugha ya kuudhi kwa sajenti John na kunukuu kauli zilizotolewa na Bulaya kwamba alisema, “Wewe m...., kibaraka wa CCM unakaa nyumba za bati mshahara Sh70,000  wewe sajenti  fungua geti.”

Wakili Martine amedai katika shtaka la sita linalomkabili Jacob naye alitamka maneno yaliyosababisha uvunjifu wa amani.

“Wewe m..., acha kugombana na wanawake gombana na mimi mwanaume kibaraka wa CCM fungua geti wewe,” amesema Martine akimnukuu Jacob.

Pia,  Jacob anakabiliwa na shtaka la shambulio  tukio analodaiwa kulifanya katika gereza hilo.

Wakili Martin amedai Jacob akiwa kwenye gereza hilo anadaiwa kumshambulia sajenti John kwa kumvuta shati lake na kulichana  wakati akitekeleza majukumu yake.

Washtakiwa walikaana mashtaka yao na upande wa mashtaka kudai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 23, 2020 itakapoitwa kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz