Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO:Maktaba ya bilioni 90 chuo kikuu yakosa watumiaji

Video Archive
Tue, 3 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wahenga waliosema “penye miti hapana wajenzi” hawakukosea. Msemo huu unasadifu kinachoendelea sasa kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa maktaba mpya iliyojengwa hivi karibuni chuoni hapo na kugharimu kiasi cha Sh90 bilioni, haitumiwi ipasavyo na walengwa.

Maktaba hiyo ya kisasa iliyofunguliwa Novemba 27, 2018 ina uwezo wa kuchukua watu 2,100 kwa wakati mmoja, ikiwa na kompyuta 160 zilizounganishwa na intaneti na ina chumba cha mikutano kinachotosha watu 600.

Ili kikidhi mahitaji ya watumiaji, Serikali ilitenga Sh1.78 bilioni kwa mwaka 2017/18 kwa ajili ya ununuzi wa vitabu ambavyo vinatakiwa vichangie kujaza makabati yenye uwezo wa kuchukua vitabu 800,000.

Lakini jitihada hizo za Serikali, ambayo ilishirikiana na China kujenga jengo hilo, zinaonekana kutopokelewa vizuri na walengwa, ambao ni wanafunzi na watu wengine wanaofanya shughuli kama utafiti.

“Idadi ya wanafunzi wanaojitokeza kusoma, hailingani na uwezo wa maktaba hii ya kisasa na ya kipekee si tu kwa Tanzania, bali hata kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara,” anasema Ernest Nyari, mkutubi msaidizi wa maktaba hiyo.

Pia Soma

Advertisement   ?
“Kwa sasa naweza kusema haijawa full utilized (haijatumika kikamilifu), ila nina uhakika mwaka mpya wa masomo utakapoanza maktaba itajaa, maana wanafunzi watakuwa na uelewa wa kutosha wa huduma zinazopatikana.’’

Kwa mujibu wa Nyari hali hiyo inawezekana ikawa imesababishwa na wanafunzi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu rasilimali za kimasomo zilizomo katika maktaba hiyo.

Ni kwa kuliona hilo, anasema uongozi ulianza utaratibu wa kuwaonyesha walimu wa idara zote za chuoni hapo kuhusu yaliyomo ndani ya maktaba hiyo.

“Tulianza kuwapa ufahamu walimu ili wakawe mabalozi kwa wanafunzi wao kuwaeleza vitu vilivyopo ndani ya maktaba hii ya kisasa. Lengo letu kwa sasa ni kuwafikia wanafunzi waje kujionea,” alisema.



Chanzo: mwananchi.co.tz