Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Mabadiliko ya viongozi wa serikali yaliyofanywa na Rais Magufuli

Video Archive
Mon, 3 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa makatibu wakuu na makamishna wa wizara na vyombo vya ulinzi na usalama, akiwemo Christopher Kadio aliyekuwa katibu tawala wa mkoa wa Mwanza kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mabadiliko hayo yamekuja kufuatia kuenguliwa kwa viongozi wa wizara hiyo akiwemo aliyekuwa Waziri Kangi Lugola na aliyekuwa Kamishna Jenerali wa jeshi la Zima moto na Uokoaji, Thobias Andengenye Januari 23, baada ya Rais Magufuli kuibua kashfa ya mkataba wa jeshi hilo aliosema ni wa hovyo.

Awali Katibu mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali Jacob Kingu alijiuzulu kabla ya kuteuliwa kuwa balozi.

Akizungumza jana Ikulu ya Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk John Kijazi alisema pia Rais Magufuli amemteua John William Masunga kuwa Kamishna wa Zimamoto na uokoaji, huku Brigedia Jenerali Suleiman Munyiya kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania akiteuliwa kuwa Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza.

Dk Kijazi pia alisema Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbas kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alimtaja pia Mary Makondo aliyekuwa kamishna katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akisema sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo

Pia Soma

Advertisement
“Rais pia amemteua Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara ambaye ni Profesa Riziki Shemdoe. Kabla ya uteuzi huo alikuwa katibu tawala mkoa wa Ruvuma,” alisema.

Alimtaja aliyekuwa Katibu tawala wa mkoa wa Tanga, Zena Ahmed Said akisema kuwa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wizara ya Nishati, huku pia akimteua aliyekuwa Kamishna wa Umeme wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Leonard Masanja kuwa Katibu mkuu wa wizara hiyo.

Mbali na makatibu hao, Rais Magufuli pia ameteua makatibu tawala ambapo Mkoa wa Tanga ameteuliwa Judika Omari, Mkoa wa Ruvuma, Streven Mashauri na Mkoa wa Mwanza akiteuliwa Emmanue Tukuba.

Kwa upande wa makamishna, Dk Kijazi alimtaja Mathew Mhonge aliyeteuliwa kuwa Kamishna wa Ardhi katika wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kwa upande wa Mahakama, Dk Kijazi alisema Rais Magufuli amemteua Wilbert M chuma Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Kelvin D Mhina kuwa Msajili Mahakama ya rufani na Samira Sarwat kuwa Msajili wa Mahakama Kuu.

Pia, Rais ameteua makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ambao ni pamoja na Jaji Gerald Ndika, Wakili Julius Bundala na Wakili Genoveva Kato.

Chanzo: mwananchi.co.tz